(+Video) Jamaa kutoka Bungoma anayedai kuwa mjukuu wa Kibaki avuruga misa ya mazishi

Muhtasari

•Allan Makana alimkimbilia Askofu Mkuu Martin Kivuva punde tu baada ya hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta akiomba muda mfupi wa kuzungumza.

Jamaa aliyesababisha taharuki bungeni huku akidai kwamba ni mjukuu wake hayati Mwai Kibaki
Image: EZEKIEL AMING'A

Jamaa mmoja kutoka Bungoma anayejitambulisha kama mjukuu wa Kibaki alivuruga ibada ya misa ya Kibaki kwa muda baada yake kujitokeza jukwaani bila kualikwa.

Allan Makana ambaye alisababisha kizazaa kikubwa nje ya bunge siku ya Jumanne leo hii alimkimbilia Askofu Mkuu Martin Kivuva punde tu baada ya hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta akiomba muda mfupi wa kuzungumza.

"Nahitaji dakika mbili tu kutoa maneno machache. Dakika mbili tu nataka kusema kitu," alisikika akisema.

Hata hivyo, mtumishi huyo wa Mungu alipuuzilia ombi lake kwa upole na kuwaelekeza wasimamizi wa misa kumsindikiza polepole kutoka jukwaani.

"Yeye ni mtoto wa taifa letu ambaye amewezwa na hisia kwa kumpoteza rais wetu. Tafadhali mtendee mema," Kivuva alihimiza.

Tazama:-

Askari waliokuwa wamesimamia ibada walimfurusha jamaa huyo kwa haraka kabla yake kusababisha kizazaa zaidi. 

Siku ya Jumanne, Makana aliangua kilio kikubwa na kuvua nguo  nje ya majengo ya bunge  akidai kuwa yeye ni mjukuu wa Kibaki.

“Mbona umeenda haraka hivi,” Makana alisikika akisema huku machozi yakimdondoka kwenye mashavu.

Makana alipohojiwa kuhusiana na kisa hicho alisema polisi walimkamata na kumpeleka kituoni. Pia alidai kuwa alipoteza kazi yake baada ya tukio hilo.

“Walinipeleka kituo cha polisi kisha jioni wakanihamishia kituo kikuu cha polisi, nilibaki pale na kupelekwa City Hall kwa ajili ya kuleta fujo siku iliyofuata, sikuona kosa nililofanya hata faili langu. hakuwepo." Makana alisema katika mahojiano na Standard.