Jimmy Kibaki apuuzilia mbali madai ya kuunga mkono muungano wa Kenya Kwanza

Muhtasari
  • Baadhi ya Wakenya walishiriki ujumbe huo wakiwapotosha Wakenya kwamba Jimmy amejiunga na kambi ya DP
JImmy KIbaki
Image: EZEKIEL AMINGA

Madai kuwa mwanawe hayati Mwai Kibaki Jimmy anaunga mkono muungano wa Kenya Kwanza Alliance unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto ni ghushi.

Ripoti hizo ziliibuka mara ya kwanza kutoka kwa akaunti ya Twitter ambayo ina jina la "Jimmy Kibaki HSC".

Baadhi ya Wakenya walishiriki ujumbe huo wakiwapotosha Wakenya kwamba Jimmy amejiunga na kambi ya DP.

Kando na hayo, Jimmy ameithibitishia Radiojambo kwamba yeye si mwanachama wa Muungano wa Kenya Kwanza.

"Imenifikia kwamba kuna akaunti kadhaa za uwongo za Twitter zinazoniiga, na zinazodaiwa kuashiria kwamba ninaunga mkono muungano wa kisiasa wa Kenya Kwanza," Alisema.

"Ningependa kuchukua fursa hii kuwafahamisha Wakenya kwamba wanapaswa kupuuza matangazo yote ghushi na ya kihuni yanayotoka kwa walaghai hawa."

Jimmy alibainisha kuwa anafurahia uhusiano mzuri na Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu na kuongeza kuwa uaminifu wake kwake hauna shaka.

Hata hivyo, alikataa kutaja anaemuunga mkono nani kwa urais akisema atakayempigia kura ni mambo yake binafsi.

"Mkenya yeyote mwenye fikra sahihi ambaye anaelewa uhusiano wa miaka 62 kati ya familia ya Kenyatta na Kibaki atajua kwamba uaminifu wangu kwa Rais Uhuru Kenyatta ni mtakatifu, na urafiki wetu wa miaka 50 unadumu," alisema.