Licha ya kuzawadiwa miaka 5 iliyopita 'Githeri man' akiri maisha yake hajakubadilika

Muhtasari

•Githeri Man aligonga vichwa vya habari baada ya kupigwa picha akiwa amebeba 'githeri' kwenye mfuko wa plastiki huku akisubiri kupiga kura.

•Kamotho aliweka wazi kuwa licha ya kupewa msahada, hayo yote yamemfanya kuwa maskini zaidi kwani hakuna aliyetoa suluhisho la kudumu au kumshauri baadaye.

George Mugo, KWA HISANI
George Mugo, KWA HISANI
Image: Githeri man

Martin Kamotho, almaarufu 'Githeri Man' amejitokeza na kusema kuwa tangu agonge vichwa vya habari wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2017 maisha yake duni haijabadilika.

Mwanaume huyo aligonga vichwa vya habari baada ya kupigwa picha akiwa amebeba 'githeri' kwenye mfuko wa plastiki huku akisubiri kupiga kura.

''Hakuna kitu ambacho kimeboreshwa katika maisha yangu tangu 2017. Watu wote walionitakia heri na watu ambao walipiga picha na mimi miaka mitano iliyopita wametoweka na sijui waliko,'' Kamotho alisema.

Umaarufu wake katika mitandao mbalimbali ya kijamii ulimletea mafanikio kwani alizawadiwa kipande cha ardhi huko Karen na Ngong Crescent  shamba lililogharimu Ksh 269,000.

Hapo awali aliishi Kayole,pia alipokea kifurushi cha usafiri kilicholipwa kwa ajili yake na familia yake kuelekea Maasai Mara.

Safaricom pia ilimzawadia Samsung S8+ yenye thamani ya Ksh 100,000 pamoja na mkewe.Mtoto wake wa pekee pia alizawadiwa Tecno Canon yenye thamani ya Ksh 50,000.

Githeri Man pia alisema alialikwa kula chakula cha mchana Ikulu, na mara ya pili alipoalikwa,  alidai kupewa Ksh 150,000 na Serikali kama tuzo na tangu wakati huo, hajawahi kwenda Ikulu tena.

Kamotho aliweka wazi kuwa licha ya kupewa msahada na mashirika mbali mbali, alidai kuwa hayo yote yamemfanya kuwa maskini zaidi kwani hakuna aliyetoa suluhisho la kudumu au kumshauri baadaye.

Baba huyo alikumbuka venye  picha yake ilipoanza kuvuma mtandaoni watu walikuja kumtafuta jambo ambalo lilimtia hofu na  alilazimika kujificha nyumbani kwa shangazi yake.