Elizabeth Manyalo, mke wa mwanaume aliyejichoma moto azungumza kuhusu ndoa yao

Kulingana na ripoti ya polisi, waliweza kubaini kwamba wawili hao walikuwa na ugomvi ndani ya gari

Muhtasari

•Kulingana na ripoti ya polisi, waliweza kubaini kwamba wawili hao walikuwa na ugomvi ndani ya gari kabla ya mwanaume huyo kumdunga mkewe na kisu.


Elizabeth akizungumza na wanahabari
Elizabeth akizungumza na wanahabari
Image: HANDOUT

Elizabeth Munyalo, mke wa marehemu Dennis Musyoka aliyefariki baada ya kuteketeza gari akiwa ndani na bintiye wa miaka 2 katika eneo la Nasra Estate, Kaunti ya Nairobi Jumapili tarehe 22, amefichua kuwa marehemu alikuwa mtu ambaye alipenda vurugu na hiyo ndo  ilikuwa moja ya sababu ya wao kutengana.

Akizungumza baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, Munyalo alisema kuwa wamekuwa wakipigana kuhusu malezi ya binti yao wa miaka 2 baada ya kutengana.

"Tulikuwa na changamoto kwenye ndoa tangu mwaka jana na tukaamua kusitisha uhusiano wetu. Baada ya kuhama, aliamuru nimrudishie mtoto baada ya vitisho vingi, lakini  niliamua kumruhusu amuone mtoto. Alikasirika baada ya kumwarifu kwamba sitapatikana Jumamosi siku ambayo  binti yangu alifaa kusherehekea kuzaliwa kwake.Kwa hivyo nilipochukua mtoto Jumapili, aliniambia kuwa angetuua sote akiwemo mtoto mchanga,”Munyalo alisema.

Kulingana na ripoti ya polisi, waliweza kubaini kwamba wawili hao walikuwa na ugomvi ndani ya gari kabla ya mwanaume huyo kumdunga mkewe na kisu.

Mama huyo alifanikiwa kutoroka baada ya kupiga nduru na kupata msaada kutoka kwa raia wema waliomkimbiza hospitali ya Mama Lucy, huku mumewe Dennis akijifungia ndani ya gari na mtoto wao wa kike mwenye umri wa miaka 2 na kuchoma gari hilo.

Wasamaria wema walifanikiwa kumtoa binti huyo kwenye gari na kumkimbiza katika hospitali ya Mama Lucy na baadaye kufariki dunia alipokuwa akihamishiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.