Ekuru Aukot ataka maombi ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaharamishwa

Maneno hayo yalipingwa vikali na jaji mkuu mstaafu Willy Mutunga.

Muhtasari

• “Kuharibu muda wa Wakenya katika masuala ya kesi hovyo au maombi yasiyo na tija yanafaa kuharamishwa,” Aukot aliandika.

Kinara wa Thirdway Alliance
Dkt Ekuru Aukot Kinara wa Thirdway Alliance
Image: Twitter

Mtandao wa Twitter nchini Kenya una umaarufu kama jukwaa la watu kurushiana checvhe kali haswa kuhusu masuala ya kisiasa kwa njia ya kitaalamu bila kushirikisha hasira za vijiweni.

Kiongozi wa chama cha Thridway Alliance Ekuru Aukot amekuwa wa hivi punde kujipata katika majibizano makali na wasomi wa sheria kweney Twitter baada ya matamshi yake ya kutaka maombi mengine ya kupinga matokeo ya uchaguzi kuharamishwa ili kuokoa muda.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Aukot alikuwa ametoa wazo kwamba maombi ya kubatilishwa kwa ushindi wa rais mteule William Ruto ni kama kuharibu muda wa wakenya katika kile alisema kwamba maombi hayo ni hovyo na yanafaa kuharamishwa ili kuokoa muda na pesa za mkenya mlipa ushuru.

“Kuharibu muda wa Wakenya katika masuala ya kesi hovyo au maombi yasiyo na tija yanafaa kuharamishwa,” Aukot aliandika.

Hapo hapo watu kadhaa walifurika na kuchukua pande zao kinzani huku wengi wakionekana kumuapiza vikali kuhusu utafsiri wake wa kesi kama hizo kwani yeye alikuwa mmoja wa jopo lililopendekeza na kuwasilisha katiba ya mwaka 2010.

Aliyekuwa jaji mkuu Willy Mutunga alikuwa miongoni mwa wale walioshtushwa na matamshi hayo ambayo hayakutarajiwa kutoka kwa mtu mweney busara zake kama Aukot na hakusita kumpa makavu yake mubashara.

“Anasema aliyekuwa katibu mkuu wa kamati ya wasomi waliotupatia katiba ya 2010. Inatia huruma sana. Kabisa umepotoshwa. Ombi la mahakamani linatafuta suluhu mahakamani. Iweje hilo liharamishwe? Hii ni miiko ya ufashisti,” Mutunga alifoka vikali kwa kejeli kubwa.

Aukot hakuonekana kuyumbishwa na cheche hizo kwani alisimama nafasi yake tisti na kusema kwamba hivi karibuni Wakenya ambao kwa sasa wanamsimanga kwa kile alisema ni ukweli watarudi kumshukuru kwani yeye ameona mbali tayari.

Awali Aukot alikuwa amebashiri kwamba Ruto angemshinda Raila jambo ambalo alikuja kujipiga kifua kwamba lilitokea jinsi alivyolibashiri.

Aukot alikuwa miongoni mwa wale waliotegemea kuwania urais katika kinyang’anyiro cha Agosti 9 kabla ya shoka la tume ya IEBC kumpata barabara na kumkata nje.