Ekuru Aukot azuiwa kuwania urais baada ya kukosa kuwasilisha saini na vitambulisho vya wafuasi

Muhtasari

•Aukot amekosa kupatiwa kibali baada ya kushindwa kuwasilisha nakala za vitambulisho vya wapiga kura 48,000 ambao walimuidhinisha.

•Mwenyekiti wa IEBC Ekuru Aukot azuiwa kuwania urais baada ya kukosa kuwasilisha saini na vitambulisho vya wafuasi

IEBC imekataa ombi la Ekuru Aukot kuwania urais katika kinyang'anyiro cha mwezi Agosti
IEBC imekataa ombi la Ekuru Aukot kuwania urais katika kinyang'anyiro cha mwezi Agosti
Image: IEBC

Tume ya IEBC imemzuia mgombea urais wa Thirdway Alliance Dkt Ekuru Aukot kuwania kiti hicho katika kinyang'anyiro cha mwezi Agosti.

Aukot amekosa kupatiwa kibali baada ya kushindwa kuwasilisha nakala za vitambulisho vya wapiga kura 48,000 ambao walimuidhinisha.

IEBC imetangaza kuwa mwanasiasa huyo pia alikosa kutimiza idadi ya saini za wafuasi zinazohitajika ili kupatiwa kibali cha kuwania urais.

"Msimamizi wa Uchaguzi wa Urais Wafula Chebukati amekataa ombi la Mgombea Urais wa Thirdway Alliance Kenya Dkt. Ekuru Aukot. Hii ni baada ya kushindwa kutoa nakala za vitambulisho vya wafuasi wake," IEBC ilitangaza kupitia taarifa.

"Dkt Aukot pia alishindwa kutimiza idadi ya chini ya saini za wafuasi wake, ambazo zinahitajika ili kusajiliwa kama Rais."

Mwenyekiti wa IEBC pia alidai kuwa cheti cha shahada cha Aukot kilikosa saini ya chuo ambacho alisomea.

Aukot alikuwa anajaribu bahati yake kukalia wadhfa wa juu zaidi nchini kwa mara ya pili baada ya kubwagwa chini katika uchaguzi wa 2017.

Huku akijitetea, Aukot amedai kuwa Wakenya wengi hawapo tayari kupatiana vitambulisho vyao kwa ajili ya kutoa nakala.

"Tulifanya makusudi kutoleta saini. Watu wanataka kuhongwa ili wakupe vitambulisho vyao  utoe nakala," Aukot aliambia IEBC.

Mgombea urais huyo aliapa kuenda mahakamani kulalamika dhidi ya hitaji la saini na nakala za vitambulisho vya wafuasi ili kuidhinishwa kuwania urais.

Jumapili asubuhi IEBC ilimuidhinisha mgombea urais wa Azimio la Umoja- One Kenya Raila Odinga kuwania kiti hicho.