DCI kuwasilisha ushahidi mkubwa unaohusisha Barasa na mauaji ya mlinzi wa mpinzani wake

Wapelelezi wanaoshughulikia kesi hiyo walibaini kuwa risasi iliyotumika kutekeleza mauaji ilitoka kwa bastola ya mbunge huyo.

Muhtasari

•DCI imeripoti kuwa uchunguzi wa silaha katika maabara ya kitaifa ya silaha umehusisha bastola ya Barasa na risasi iliyomwangamiza mlinzi huyo.

•Mbunge huyo ambaye amekuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi ameratibiwa kujibu mashtaka ya mauaji katika mahakama ya Kakamega.

Image: FACEBOOK// DCI

Kitengo cha DCI kimesema wamekusanya ushahidi mkubwa unaomhusisha mbunge mteule wa Kimilili Didmus Barasa na mauaji ya Brian Olunga.

Olunga ambaye alihudumu kama mlinzi wa mgombea ubunge wa Kimilili kwa tiketi ya DAP-K Brian Khaemba alipigwa risasi na kuuawa mnamo siku ya uchaguzi katika kituo cha kupigia kura cha Chebukwabi.

Kufuatia tukio hilo, mkuu wa DCI George Kinoti alimuagiza mbunge huyo ambaye alikuwa ameingia mitini kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi huku wapelelezi wakiendeleza uchunguzi zaidi.

"Tangu wakati huo timu maalumu ya wapelelezi kutoka tawi la mauaji, uhalifu wa kidijitali na vitengo vya uchunguzi wa  eneo la uhalifu wa kiforensiki wamefanya uchunguzi wa kina na kumweka Mhe Barasa kwenye eneo la mauaji," DCI imesema katika taarifa.

Kitengo hicho pia kimeripoti kuwa uchunguzi wa silaha katika maabara ya kitaifa ya silaha umehusisha bastola ya Barasa na risasi iliyomwangamiza mlinzi huyo.

Ripoti ya wapelelezi wanaoshughulikia kesi hiyo iliashiria kuwa risasi iliyotumika ambayo ilipatikana katika eneo la tukio ilitoka kwa bastola ya mbunge huyo.

"Zaidi ya hayo, ripoti ya uchunguzi wa maiti ya mwanapatholojia wa serikali ilitoa maoni kwamba chanzo cha kifo kilikuwa jeraha kubwa la kichwa lililosababishwa na risasi. Wakati wa uchunguzi wa maiti, vipande vya risasi pia vilitolewa kutoka kwa ubongo wa marehemu," Taarifa ya DCI imesema.

Kitengo hicho sasa kimeeleza kuwa wako tayari kuwasilisha ushahidi mkubwa dhidi ya Barasa ambao wamekusanya katika kipindi cha uchunguzi.

Mbunge huyo ambaye amekuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi ameratibiwa kujibu mashtaka ya mauaji katika mahakama ya Kakamega.