Mtoto wa miaka 3 aanguka kutoka ghorofa ya nane, Tassia

Alitua kwenye ghorofa ya chini kwa kichwa na kufariki papo hapo.

Muhtasari

• Kamanda wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alitaja tukio hilo la kusikitisha na kusema wameanzisha uchunguzi.

 

Crime Scene
Image: HISANI

Mtoto mdogo mwenye umri wa miaka mitatu alianguka kutoka orofa ya nane ya jengo eneo la Tassia, Nairobi na kufariki papo hapo.

Msichana huyo aliyetambulika kwa jina la Blessing Mumo alikuwa akicheza kwenye ngazi ya jengo hilo pamoja na watoto wengine alipoteleza.

Alitua kwenye ghorofa ya chini kwa kichwa na kupata majeraha mabaya.

Majirani waliosikia kishindo hicho walikimbilia kumuokoa na kumpeleka katika Hospitali ya Forces Memorial ambako alitangazwa kufariki.

Kamanda wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alitaja tukio hilo la kusikitisha na kusema wameanza uchunguzi.

Alisema ajali hizo zimekuwa zikiripotiwa jijini huku kukiwa na wito wa kuwekwa hatua za kiusalama ili kuzishughulikia.

Kwingineko, mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 44 ulipatikana kwenye Barabara kuu ya Uhuru karibu na Hoteli ya Laico Regency Jumatatu usiku, mwathiriwa alitambulika kwa jina la Andrew Tabu.

Polisi walisema kuwa waliarifiwa na walinzi waliokuwa wakilinda hoteli hiyo kuwa maiti ya marehemu ilikuwa imelazwa katika eneo la tukio.

Bado haijabainika kilichosababisha kifo cha mwanamume huyo, mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema.

Alisema maiti hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho.