Rais Ruto atetea safari zake nyingi za nje

Ruto alisema ni kupitia safari hizo ambapo ameweza kupata mikataba kadhaa kwa ajili ya nchi

Muhtasari

•Rais alibainisha kuwa ziara yake ya hivi majuzi nchini Saudi Arabia ilimwezesha kupata nafasi za ajira kwa Wakenya 350,000 .

•Mapema wiki hii, Mkuu wa Nchi alikuwa Saudi Arabia kwa toleo la 7 la Mkutano wa Future Investment Initiative (FII).

Rais wa tano wa Kenya
WILLIAM RUTO Rais wa tano wa Kenya
Image: Facebook//WILLIAMRUTO

Rais William Ruto ametetea safari zake nyingi nje ya nchi tangu ashike mamlaka.

Akitoa hotuba yake wakati wa ibada ya kanisa katika kaunti ya Uasin Gishu mnamo siku ya Jumapili, rais Ruto alisema ni kupitia safari hizo ambapo ameweza kupata mikataba kadhaa kwa ajili ya nchi.

Baba wa taifa alitoa  mfano akibainisha kuwa ziara yake ya hivi majuzi nchini Saudi Arabia imemwezesha kupata nafasi za ajira kwa Wakenya 350,000 huku mkataba wa nchi mbili ukitarajiwa kutiwa saini katika muda wa wiki tatu zijazo.

Ruto alifichua kuwa atasafiri kuenda katika nchini hiyo tena kwa ajili ya kutia saini mkataba huo katika muda wa wiki tatu zijazo.

"Kuna watu wananipigia makelele mbona umeenda safari hii, hiyo ndio kazi yangu ya Rais, mimi ndio chief agent wa  Kenya, mimi ndio balozi wa Kenya wa kupanga vile Kenya itasonga mbele," alisema.

Wakenya wengi wamekosoa safari nyingi za nje za rais tangu achukue vazi la uongozi. Wikendi hii tu, Ruto alikuwa Congo kuhudhuria Mkutano wa Tatu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Mabonde Matatu. Hii ilikuwa safari ya 39 ya Rais Ruto tangu ashike wadhifa wake mwaka jana Septemba.

Mapema wiki hii, Mkuu wa Nchi alikuwa Saudi Arabia kwa toleo la 7 la Mkutano wa Future Investment Initiative (FII).

Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alikosoa ziara za Ruto katika mataifa tofauti kutokana na changamoto za kiuchumi na gharama ya juu ya maisha.

Alipendekeza kuwa ingefaa zaidi ikiwa Ruto atasafiri kwa masuala muhimu tu, huku masuala mengine mengi yakishughulikiwa na Makatibu wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na masuala ya kigeni au Waziri wa Biashara.

Alisema rais husafiri na timu kubwa ya watu, inayohusisha vifaa vingi vya usafirishaji. “Kwa kuwa thamani ya dola kwa sasa imefikia Sh150.

Hata hivo Mbunge wa Eldas Adan Keyna ametetea safari za  rais Ruto akisema yeye ndiye mwanadiplomasia mkuu nchini.

Akizungumza siku ya Alhamisi wakati wa onyesho la Citizen asubuhi, mbunge huyo alisema chochote anachofanya rais ni kwa manufaa ya Wakenya. Alisema ziara na safari zake zote nje ya nchi ni kwa ajili ya kunufaisha uchumi wa nchi.