Mauaji ya Thika, polisi wamkamata mshukiwa JKIA akijaribu kuondoka Kenya

Inasemekana mshukiwa alinaswa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta alipokuwa akijaribu kutoroka nchini Kenya.

Muhtasari

• Alizuiliwa katika uwanja wa ndege kabla ya kikosi cha maafisa kutoka Kasarani na makao makuu ya DCI kumchukua ili kuhojiwa.

Picha za uchunguzi zilinasa mshukiwa nje ya jumba huko Roysambu Jumamosi Januari 13, 2024.
Picha za uchunguzi zilinasa mshukiwa nje ya jumba huko Roysambu Jumamosi Januari 13, 2024.

Maafisa wa upelelezi siku ya Jumanne walikuwa wakimhoji mwanamume wanayeamini kuwa alimuua mwanamke ambaye mwili wake uliokuwa umekatwakatwa ulipatikana kwenye jaa la taka jijini Nairobi.

Inasemekana mshukiwa alinaswa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta alipokuwa akijaribu kutoroka nchini.

Alizuiliwa akisubiri kutambuliwa na kuhojiwa, duru katika idara ya polisi zilisema.

"Ni mapema mno kusema kama yeye ndiye mtu anayesakwa kuhusu mauaji au la. Inabidi tusubiri,” afisa mmoja wa polisi alisema.

Alizuiliwa katika uwanja wa ndege kabla ya kikosi cha maafisa kutoka Kasarani na makao makuu ya DCI kumchukua ili kuhojiwa.

Viungo na mikono ya mwanamke huyo vilikuwa vimekatwakatwa na kuwekwa kwa karatasi ya plastiki na kuviringishwa kwenye shuka la kitanda.

Imebainika mwanamume huyo alitumia msumeno kuukata mwili wa mwanamke huyo ambaye kichwa chake bado hakijapatikana.

Polisi wanashuku kuwa mwanamume huyo alikuwa amekodishwa na huenda alibeba kichwa cha marehemu kuthibitishia waliyomtuma kwamba alikuwa amekamilisha kazi.

Kwa kutumia picha za CCTV, na simu, polisi wamemweka mshukiwa katika eneo la Ruaka, Kaunti ya Kiambu ambako anaonekana kukaa kwa siku nyingi.

Wapelelezi walitembelea eneo la mkasa Jumatatu na kuomba picha za CCTV kwenye majengo kadhaa kama sehemu ya uchunguzi.

Familia ya mwanamke alyeuawa (ambaye utambulisho wake haujawekwa wazi) walitembelea chumba cha kuhifadhia maiti cha City, Nairobi siku ya Jumatatu na kumtambua.

ya kutisha kuhusu mauaji ya mwanamke TRM DRIVE
Maelezo ya kutisha kuhusu mauaji ya mwanamke TRM DRIVE
Image: WILLIAM WANYOIKE

Hata hivyo, kwa sababu sehemu muhimu za mwili hazikuwepo, walitakiwa kusubiri uchunguzi zaidi wa sampuli zilizokusanywa kutoka kwa mwili huo na ndugu wa karibu kabla hawajatoa taarifa yoyote juu yake.

Sababu ya tukio hilo bado haijajulikana, polisi walisema na kuongeza mshukiwa aliukata mwili wa mwanamke huyo na kuondoa viungo, mikono na kichwa kutoka kwenye kiwiliwili.

Kisha akafunga sehemu za mwili katika shuka na mfuko wa plastiki.

Kulikuwa na alama za msumeno kwenye mwili wakati polisi walipofika kuuchukua katika chumba cha kuhifadhia maiti. Pia ilibainika kuwa mwanamume huyo alikuwa amepiga simu ili kupanga chumba hicho kwa kutumia nambari ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mwanamke. 

Polisi wanasema mshukiwa huyo alipiga simu Jumamosi, Januari 13, saa tatu usiku kukodi chumba. Baada ya kukitazama kile chumba, alirudi dakika tano baadaye.Alirudi kwa wakala huyo ambaye alimtaka alipe Sh2,000 za usiku huo kupitia malipo ya simu ya mkononi lakini akasema akaunti yake ya simu ilikuwa na matatizo na angelipa tu pesa taslimu.  

Alimpigia simu mwenye nyumba tena na kumpa mhudumu simu aongee naye ili aruhusiwe kulipia chumba hicho kwa pesa taslimu, jambo ambalo limeonekana kuwa mbinu nyingine aliyotumia kuficha utambulisho wake, polisi walisema. 

Mwanamke aliwasili saa mbili usiku na kuwaambia walinzi kuwa anaungana na mshukiwa katika Jumba la Green House Apartment chumba B1. Kulingana na polisi na wasimamizi katika ghorofa hiyo, alitarajiwa kurudisha funguo Jumapili asubuhi lakini hakufanya hivyo.