Rais Samia amuomboleza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Kenya, Jenerali Francis Ogolla

Samia alibainisha kuwa alipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kuzitaka roho za marehemu zipumzike kwa amani.

Muhtasari

•Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameungana na Wakenya kumuomboleza marehemu Jenerali Francis Ogolla.

•Samia alituma risala zake za rambirambi kwa mwenzake wa Kenya, wanajeshi, familia za wanajeshi walioangamia na Wakenya kwa ujumla.

Rais Samia Suluhu wa Tanzania
Rais Samia Suluhu wa Tanzania
Image: MAKTABA

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameungana na Wakenya kumuomboleza marehemu Kamanda wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Francis Ogolla aliyefariki katika ajali ya ndege iliyotokea kaunti ya Elgeyo Marakwet siku ya Alhamisi.

Katika taarifa yake ya Alhamisi jioni, kiongozi wa nchi hiyo jirani alituma risala zake za rambirambi kwa mwenzake wa Kenya, wanajeshi, familia za wanajeshi walioangamia na Wakenya kwa ujumla.

Samia alibainisha kuwa alipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kuzitaka roho za marehemu zipumzike kwa amani.

"Nime kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla napokea wengine tisa katika ajali ya helikopta iliyotokea leo katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet," rais Samia alisema kwenye taarifa.

Aliongeza, “Natuma salamu za pole kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Mheshimiwa @WilliamsRuto, wananchi wote wa Kenya, familia, ndugu, jamaa na marafiki wa wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo. Poleni sana. Mwenyezi Mungu azilaze roho za ndugu zetu hawa mahali pema peponi. Amina.”

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Francis Ogolla alikuwa miongoni mwa maafisa wa KDF waliopoteza maisha katika ajali mbaya iliyotokea katika eneo la Sindar, lokesheni ya Kaben, tarafa ya Tot, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Maafisa wengine tisa walioaga dunia ni pamoja na Brig Swaleh Saidi, Kanali Duncan Keitany, Lt Kanali David Sawe, Meja George Benson Magondu (ambaye pia alikuwa rubani), Capt Sorah Mohamed, Capt Hillary Litali, Sajenti Mwandamizi John Kinywa Mureithi, Sajenti Cliffonce Omondi na Sajenti Rose Nyawira.

Kufuatia kifo cha Ogolla, Rais William Ruto alitangaza kipindi cha siku tatu cha maombolezo ya kitaifa kuanzia Ijumaa, Aprili 19, 2024.

Alisema katika kipindi hicho, bendera ya Kenya na ile ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jumuiya ya Afrika Mashariki na bendera za makundi yote ya kijeshi zitapepea nusu mlingoti nchini Kenya na Kenya nje ya nchi.