KOMBE LA EUROPA

Rashford apokea mkururo wa jumbe za ubaguzi wa rangi

Alikiri kuhesabu zaidi ya jumbe 70 za ubaguzi wa rangi kwenye mitandao ya kijamii punde tu baada ya kupoteza fainali ya kombe la Europa.

Muhtasari

•"Lakini niwe mweusi ama mweupe, kandanda ni kandanda. Sote tunavaa jezi inayofanana, tunapiga mpira mmoja. Nimekuwa nikicheza mchezo huu tangu niweze kutembea. Nimeumbwa kukosolewa lakini sitakubali majadiliano ya nyani, tumbili, sokwe, ndizi na msitu mnene" Rashford alisema

Marcus Rashford
Marcus Rashford
Image: Instagram

Mshambulizi wa klabu ya Manchester United alikiri kuhesabu zaidi ya jumbe 70 za ubaguzi wa rangi kwenye mitandao ya kijamii punde tu baada ya kupoteza fainali ya kombe la Europa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, mfungaji huo wa mabao 11 kwenye ligi kuu Uingereza aliwasuta wanaotia juhudi kumfanya ahisi vibaya kuliko alivyo.

"Kwa sasa nimehesabu zaidi ya jumbe 70 za matusi ya rangi kwenye akaunti zangu za mitandao ya kijamii. Kwa wale mnaotazamia kunifanya nijihisi vibaya zaidi, nawatakieni heri njema mkijaribu" Rashford aliandika.

Mchezaji huyo raia wa Uingereza alieleza kughadhabishwa zaidi haswa na mmoja kati ya waliomtumia jumbe za matusi ambaye ni mwalimu wa hesabu katika shule ya singi.

"Nimekasirika zaidi kugundua kuwa mmoja ambaye aliacha milima ya emoji za nyani kwa DM yangu ni mwalimu wa hesabu anayefunza watoto. Na anajua vizuri anaweza baguana kirangi bila kuadhibiwa" aliandika Rashford.

Alieleza mapenzi yake kwa klanu hiyo ya Manchester ambayo amechezea tangu akiwa na miaka 7. Alieleza kuwa hajakuwa akifanya vizuri msimu huu kutokana na matatizo ya kimwili ambayo amekuwa akikabiliana nayo.

Hata hivyo alieleza kuwa hiyo sio sababu ya kupoteza fainali ya Europa na kulaumu mchezo hafifu walioucheza kwenye fainali hiyo.

"Hiyo sio sababu tosha ya kutoshinda jana(Jumatano), hayukucheza vizuri kutosha na naomba radhi kuwa hatukuweza kuleta kikombe hicho nyumbani" Alisema Rashford.

"Lakini niwe mweusi ama mweupe, kandanda ni kandanda. Sote tunavaa jezi inayofanana, tunapiga mpira mmoja. Nimekuwa nikicheza mchezo huu tangu niweze kutembea. Nimeumbwa kukosolewa lakini sitakubali majadiliano ya nyani, tumbili, sokwe, ndizi na msitu mnene" aliendelea kuandika.

Kwa muda sasa wachezaji haswa katika bara Ulaya wamekuwa wakilia kubaguliwa kirangi na baadhi ya mashabiki baada ya matokeo duni. Katika msimu wa mpira bara ulaya uliotamatika hivi majuzi, wachezaji walikuwa wamechukulia mtindo wa kupiga goti moja na kuinua mkono kabla mechi kuanza kama moja ya kampeni dhidi ya ubaguzi wa rangi