Ghost Mulee ndiye kocha mpya wa Harambee Stars

Muhtasari

•Mulee atia saini mkataba wa miaka mitatu kuifunza Stars 

•Anarejea stars kwa mara ya tatu 

•Ataandaa kikosi kwa mechi dhidi ya Comoros 

Rais wa FKF Nick Mwendwa akimkabidhi jezi mkufunzi mpya wa Harambee Stars Ghost Mulee
Rais wa FKF Nick Mwendwa akimkabidhi jezi mkufunzi mpya wa Harambee Stars Ghost Mulee

Jacob Ghost Mulee ameteuliwa mkufunzi mpya wa timu ya taifa Harambee Stars kwa kipindi cha miaka mitatu.

Akikubali uteuzi wake, Mulee alisema kwamba ana matumaini kuwa kikosi cha sasa cha Stars kinauwezo wa kufuzu kwa dimba la taifa bingwa barani afrika.

Ghost ana jukumu la kuandaa kikosi cha taifa kitakacho cheza dhidi ya Comoros.

 

Rais wa shirikishola soka nchini Nick Mwendwa alisema kwamba Ghost anatarajiwa kutaja kamati yake ya kiufundi na kuanza mara moja kuandaa kikosi cha taifa.

Mulee anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi na Francis Kimanzi aliyejiuzulu siku ya Jumanne.

Ghost anarejea katika timu hiyo kwa mara tatu baada ya kuongoza Harambee Stars kati ya mwaka 2003 – 2004, na kufikisha timu ya taifa hadi fainali za dimba la taifa bingwa barani Afrika mwaka 2004 nchini Tunisia.

Alirejea tena kama mkufunzi wa Stars mwaka 2005 lakini kwa kipindi kifupi zaidi alipojiuzulu kutokana na tofauti baina yake na uongozi wa shirikisho la soka nchini.

Mulee ambaye alizaliwa mwaka 1968 alikuwa mkufunzi wa Tusker kati ya mwaka 1999 na 2009 na kushinda taji la ligi kuu nchini Kenya mara tatu. Pia amewahi kuvifunza vilabu vya APR nchini Rwanda na Young Africans ya Tanzania.

Ikitangaza kujiuzulu kwa Francis Kimanzi taarifa kutoka shirikisho la soka nchini ilisema pande zote zilikuwa zimeafikiana kusitisha mkataba baina yao.