(+video) Golikipa wa Brazil akosea jina la mpenzi wake katika mahojiano ya moja kwa moja

Mchezaji huyo kwa furaha, alimshukuru mpenzi wake kwa kusimama na yeye ila akamtaja kwa jina tofauti.

Muhtasari

• Baada ya kugundua kwamba amekosea jina, alimuomba mwanahabari kutovujisha video hiyo kwa mpenzi wake kwani mambo yatamharibikia.

Je, unaamini kwamba watu katika mahusiano ya kimapenzi wanapaswa kuitana kwa majina yao halisi ama ni vizuri kuitana majina ya kubuni ya kimahaba?

Kwa wale wengi ambao wanasema mapenzi yananoga zaidi wakati mnaitana majina ya kubuni ya kimahaba na wapenzi wao, nini kitatokea endapo mtazoea jina hilo kabisa na mpaka kulisahau jina halisi la mpenzi wako?

Hii ni hali ambayo ilimpata mchezaji mmoja wa soka ambapo katika mahojiano ya moja kwa moja, alikuwa anataka kumshukuru mchumba wake ila akasahau jina lake na kutaja jina tofauti kabisa.

Katika video ambayo imesambazwa na mwanzo iliyopakiwa na shirika la habari la Sky nchini Uingereza, golikipa wa timu ya Esperance Mbrazil Kainan alipokuwa akifanya mahojiano baada ya kipute alichotia jitihada na kutajwa kama mchezaji bora, alikosea jina la mpenzi wake.

Inaarifiwa kwamab pindi tu kipenga cha mwisho kilipopulizwa, mchezaji huyo alipiga kelele na katika utetezi wake, Kainan alikuwa na nia njema. Kipa huyo alitaka kutoa pongezi kwa mpenzi wake, labda kumshukuru kwa jukumu lake katika kazi yake au kitu kama hicho.

Basi kubweka kwake kukasikika na aliposogezewa kipaza sauti ili kuzungumza alichokuwa akikipigia kelele, Kainan alitaja jina tofauti. Inavyoonekana, jina la mpenzi wake ni Jucielly, lakini alimshukuru Grazi.

“Kwa mpenzi wangu, ambaye anafanya kazi sasa, Asante Mungu. Vinginevyo, nisingekuwa hapa. Grazi, kumbato langu linakuhusu!” alisema mchezaji huyo huku akionekana kujuta ghafla baada ya jina hilo kumtoka kinywani.

Kwa haraka mno mchezaji huyo alijirekebisha na kudokeza kwamba tayari ameshataja jina tofauti na mpenzi wake na hapo kurudia tena kuzungumza upya.

“Jucielly ... nilisema jina lisilo sahihi la mchumba wangu. Niko na uhakika! Niko na uhakika! Nitaenda kupigwa nyumbani,” alisema Kainan kwa kujuta huku pia akimtaka mwanahabari huyo kutovujisha video hiyo kwa mpenzi wake kwani hali itakuwa mbaya kwa upande wake, kando na kupigwa alikokutana pengine hata kuachwa kungemhusu video hiyo ingemfikia Jucielly.