SOKA KIMATAIFA

Haaland atarajiwa kuongoza City kushambulia Inter Juni 10

Amefunga mabao 52 katika mashindano yote huku 36 akifunga kwenye ligi ya Premier

Muhtasari

• Haaland, kwa mechi 52 katika mashindano yote, ameweza kufunga mabao 52 huku 36 akiyafunga kwenye ligi ya Premier.

• Historia ya vijana hao wa Pep kutolinyakua taji la EUFA licha ya kufika fainali msimu wa 2021, itabadilika iwapo watapata ushindi dhidi ya Inter Milan

Erling Haaland
Erling Haaland
Image: HISANI

Huku shindano la Ligi ya Mabingwa likitarajiwa kufika ukingoni msimu huu hapo kesho Juni 10,klabu ya Manchester City haijapoteza mechi yoyote katika shindano hilo msimu huu.

Kwa Mechi 12, City imecheza kufikia sasa kwenye shindano hilo, imepata ushindi mara saba na sare mara tano.

Mshambulizi Erling Haaland ndiye anayemulikwa sana na mashabiki wa kabumbu, kutokana na jinsi amekuwa akicheka na wavu msimu huu tangu ajiunge na vigogo hao wa soka Uingereza.

Haaland, kwa mechi 52 katika mashindano yote, ameweza kufunga mabao 52 huku 36 akiyafunga kwenye ligi ya Premier.

Nyota huyo mwenye uraia wa Norway ameifaa sana klabu ya City, tangu walipomsajili kutoka Borussia Dortmund msimu wa joto uliopita. Ameisadia City kulibeba taji la Premier pamoja na FA, huku akitarajiwa kuiweka historia mpya klabuni iwapo atalinyakua taji la Champions League Jumamosi hii mjini Istanbul.

Chini ya ukufunzi wa meneja Pep Guardiola, Man City wameshinda Premier League mara tano kwa misimu 6, jambo ambalo limeifanya klabu hilo kuorodheshwa kuwa miongoni mwa klabu bora ulimwenguni.

Historia ya vijana hao wa Pep kutolinyakua taji la EUFA licha ya kufika fainali msimu wa 2021, itabadilika iwapo watapata ushindi dhidi ya Inter Milan.

Licha ya hayo, Man City ina hofu kuwa huenda huenda kitumbua chao kikaingia mchanga, hasa wanapomshuku kiungo mkabaji Kyle Walker kuanza katika mechi hiyo ndipo amthibiti mshambulizi wa Argentina Lautaro Martinez.

Limebakia kuwa jambo la muda, kwa Haaland na City kuibadili historia, au mambo yataendelea kutumbukia nyongo hasa katika shindano la Champions League.

Unamtakia nani ushindi kati ya Man City na Inter Milan?