Mike Sonko amtaka Kalonzo kuungana na naibu rais William Ruto

Muhtasari

• Mike Sonko amemtaka Kalonzo kuungana na naibu rais ili kuikomboa nchi hii.

• Alisema kwamba Raila hana nia njema aye.

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Mbuvi Sonko amemtaka kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka kujiunga na chama cha UDA kinachoongozwa na naibu rais William Ruto.

Sonko alimtaka Kalonzo kujiondoa katika vuguvugu la Azimio la Umoja kwa kile alikitaja kuwa Raila Odinga hana nia njema naye.

Aidha, alishikilia kwamba ana rekodi za Odinga na naibu mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe wakipanga njama ya kumtumia na baadaye kumtelekeza.

"Niko na rekodi wakipanga njama ya kukutumia, nitakutafuta baadaye nikuonyeshe," Sonko alisema.

Kulingana na Sonko, naibu rais William Ruto ndiye kiongozi ambaye wanaweza kushirikiana ili kulikomboa taifa hili, na kufufua uchumi.

Alishikilia kwamba lengo la Raila Odinga kumvuta Kalonzo ndani ya Azimio ni kufanikisha mchakato wa kupitisha mswada wa BBI.

"Kalonzo acha nikuambie, sisi tunakuheshimu kama kiongozi wetu ndo maana nakuambia hao jamaa hawana nia nzuri na wewe," Sonko alisema.

Vilevile aliwataka magavana Alfred Mutua, Charity Ngilu na Kivutha Kibwana kuungana ili kuzungumza kwa sauti moja mbele ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.