"Sioni ubaya kujaribu kuipindua serikali!" Kuria amtetea Ruto

Muhtasari

• Mbunge wa Gatundu Kusini amemtetea Ruto dhidi ya madai ya rais Kenyatta kwamba alijaribu kuipindua serikali ya Jubilee.

• Kuria alisema Raila ndiye alikuwa wa kwanza kujaribu mapinduzi na akapandishwa cheo na hivyo kutaka Ruto pia apandishwe. 

Kiongozi wa Chama Cha Kazi, Moses Kuria
Kiongozi wa Chama Cha Kazi, Moses Kuria
Image: Facebook

Wikendi iliyopita rais Uhuru Kenyatta alimwaga mtama kuhusu kuvunjika kwa uchumba wa kisiasa baina yake na naibu wake William Ruto alipokutana na wazee wa jamii ya Agikuyu katika ikulu ya Nairobi.

Rais Kenyatta alisema kwamba naibu wake alikuwa amepanga njama ya kumng’atua madarakati lakini ikafeli baada ya kushirikiana na Raila kwenye Handshake ambayo ilitibua njama ya Ruto.

Kulingana na Uhuru, Ruto alikuwa amepanga njama ya kumuondoa mamlakani kama rais na hiyo ndio sababu kuu ya kudorora kwa urafiki wao.

Baada ya madai hayo ya rais Kenyatta kuzagaa na kuzua hisia mseto huku wakenya wakigawanyika pakubwa kutokana nayo, sasa mbunge wa nyumbani kwa Uhuru Kenyatta, Moses Kuria amejotokeza na kumtetea naibu rais dhidi ya maneno hayo.

Kuria aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema kwamba haoni ubaya wa kupanga njama ya kuing’atua madarakani serikali ambayo imefeli kufanya kazi kwa wananchi.

Pia Kuria alimtetea Ruto kwa kusema kwamba Raila ambaye kwa sasa rais kenyatta anamtetea alikuwa wa kwanza kutanga kuiangusha serikali ya Jubilee pale alipojiapisha kama rais wa wananchi.

“Ni nini kibaya kuhusu jkujaribu kung’atua serikali? Raila alijaribu hilo peupe mnamo tarehe 30 Januari 2018 katika bustani ya Uhuru Park na alipandishwa cheo na kuwa ‘ndugu yangu’ Mbona msimpandishe cheo pia Ruto?” aliandika Kuria kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Image: Twitter