Tanzia: Mgombea wa ODM auawa akijiandaa kwa uteuzi

Muhtasari
  • Thomas Okari, 38, alifariki alfajiri ya Jumatatu alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini
Thoomas Okari
Image: Magato Obebo

Mwaniaji wa kiti cha ODM katika kiti cha Wadi ya Bombaba ya Kisii alifariki Jumatatu kutokana na majeraha ya kuchomwa kisu Jumapili usiku na wavamizi waliokuwa wamejihami.

Thomas Okari, 38, alifariki alfajiri ya Jumatatu alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini.

Okari alikuwa amesafiri nyumbani kutoka Nairobi siku ya Alhamisi kwa uteuzi wa chama cha ODM kabla ya kifo chake.

Alikuwa akikodolea macho kiti cha Wadi ya Bombaba huko Bomachoge Borabu, Kaunti ya Kisii.

Jamaa na wanakijiji walisema alipata majeraha ya panga kichwani kufuatia shambulio hilo nyumbani kwake Bombaba.

Okari alipatikana akivuja damu nyingi kabla ya kukimbizwa katika hospitali ya Oasis mjini Kisii ambako alitangazwa kuwa amefariki.

Chanzo cha shambulio hilo bado hakijafahamika lakini mpwa wake, Daniel Mayaka, alisema wanashuku kujihusisha kwa mjomba wake katika siasa ni sababu inayowezekana.

Mayaka aliomba uchunguzi ufanyike haraka kuhusu mauaji hayo.

"Tunawaomba polisi wafanye uchunguzi ili kubaini wahalifu ni nani," aliwaambia wanahabari katika eneo la tukio.

Okari alikuwa amefika nyumbani kwake Bombaba saa 11 jioni siku ya Jumapili na kuelekea moja kwa moja kulala.

Muda mfupi baadaye, kundi la majambazi waliokuwa na silaha waliingia kwa nguvu ndani ya nyumba na kumshambulia, na kumsababishia majeraha mabaya kichwani.

"Walivunja mlango wa nyuma kwanza ili wapate kuingia kabla ya kumshambulia kwa mapanga. Wakati tunajibu walikuwa wametoroka," Mayaka alisema.

Mgombea ubunge wa ODM Evans Kimori alikashifu shambulizi hilo na kuzitaka vyombo vya usalama kuchunguza.

"Nilimkuta akiwa amelala kwenye damu huku akiwa amekatwa panga kichwani kote. Ilikuwa jambo la kuogofya," Kimori aliwaambia waandishi wa habari.