Itakuwa ngumu kwa Raila kupata kura za ukambani asiponichagua kuwa DP wake-Kalonzo

Muhtasari
  • Kiongozi huyo wa Wiper alisema Raila hatakosa kura za ukambani pekee bali pia zile za wafuasi wake
KINARA WA WIPER KALONZO MUSYOKA
Image: WILFRED NYANGARESI

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ameonya kuwa itakuwa vigumu kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kushinda kura za eneo la ukambani ikiwa hatamchagua kama mgombea mwenza wake.

Kiongozi huyo wa Wiper alisema Raila hatakosa kura za ukambani pekee bali pia zile za wafuasi wake wanaoenea zaidi ya eneo la Ukambani.

"Itatoa changamoto, kusema ukweli. Wapiga kura wangu wanaenea zaidi ya taifa la Kamba na Wiper," aliambia KTN News alipoulizwa kuhusu matokeo ya kutochaguliwa kama naibu wa Raila.

Makamu huyo wa Rais wa zamani, hata hivyo, alitoa imani kwamba atachaguliwa kuwa mgombea mwenza wa Raila.

Kalonzo alibainisha kuwa mchanganyiko wake na Raila ni njia ya uhakika ya urais.

“Sitaki kuhukumu mapema suala hilo lakini bado nadhani Raila Odinga, Kalonzo Musyoka ni tikiti ambayo huwezi kumshinda kwa ubora na tajriba,” alisema.