Shinikizo kwa Ruto kumtaja Waiguru kama mgombea mwenza

Muhtasari

•Zaidi ya wanachama 600 wa  Kenya Kwanza Alliance Youth League, tawi la North Rift walikutana Eldoret na kumuidhinisha Waiguru kama mgombea mwenza wa Ruto.

•Wiki jana vijana kutoka Nakuru walitaka muungano wa Kenya Kwanza kumchagua Waiguru kuridhi nafasi ya Ruto.

SHINIKIZO LA VIJANA: Wanachama wa Ligi ya Vijana ya North Rift Kenya Kwanza katika mkutano Eldoret Aprili 25
SHINIKIZO LA VIJANA: Wanachama wa Ligi ya Vijana ya North Rift Kenya Kwanza katika mkutano Eldoret Aprili 25
Image: MATHEWS NDANYI

Shinikizo linaendelea kuongezeka kwa Naibu Rais William Ruto kumchagua Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kama mgombea mwenza wake'

Zaidi ya wanachama 600 wa  Kenya Kwanza Alliance Youth League, tawi la North Rift walikutana Eldoret na kumuidhinisha Waiguru kama mgombea mwenza wa Ruto.

Wakiongozwa na Beverlyne Chebii, walisema Ruto atakuwa ameweka historia kwa kumteua Waiguru kuwa mgombea mwenza wake kwa sababu anathaminiwa kama kiongozi mwanamke na mtumishi wa umma mwenye uzoefu.

"Waiguru amedhihirisha uwezo wake wa kuongoza wakati alipokuwa serikalini, kupanda hadi ngazi kutoka kuwa waziri na kuwa gavana wa Kirinyaga," Chebii alisema.

Alisema Waiguru ni maarufu nchini kote na UDA tayari imenufaika kutokana na umaarufu wake katika eneo la Mlima Kenya.

"Tumezingatia mambo yote na kulinganisha wale wote waliopendekezwa kama wagombea wenza katika Kenya Kwanza. Tunapata Waiguru anafaa na anastahili nafasi hiyo,” Chebii alisema.

Wengine waliotajwa kuwa wanaweza kuwa wagombea mwenza ni pamoja na wabunge Ndindi Nyoro, Alice Wahome, Rigathi Gachagwa na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, miongoni mwa wengine.

Vijana wa North Rift pia wanasema Kenya iko tayari kwa mwanamke kushika nafasi ya naibu rais , hivyo basi, msukumo wao wa kutaka Waiguru awe debeni na Ruto katika uchaguzi wa Agosti 9.

“Wanawake wa Kenya wametoka mbali na ni watu kama Gavana Waiguru ambao wamekuwa mstari wa mbele. Kwa kutambua juhudi zao, tunahisi anafaa kuwa naibu wa rais huku tukihamasisha uungwaji mkono kwa Ruto," Chebii alisema.

Wiki jana vijana kutoka Nakuru walitaka muungano wa Kenya Kwanza kumchagua Waiguru kuridhi nafasi ya Ruto.

Kikundi hicho wakiwemo viongozi wa vijana kutoka kote nchini, kimetaja uongozi wa 'mabadiliko' wa Waiguru kuwa chanzo cha kuzingatiwa.

"Anne Waiguru anafaa kuteuliwa sio tu kwa sababu yeye ni mwanamke, lakini kwa sababu anastahili kuhudumu katika wadhifa wa naibu rais zaidi ya watangulizi wake wote. Ana rekodi ya utendaji," taarifa ya ligi ilisoma.

"Gavana Waiguru anafurahia uungwaji mkono wa Mlima Kenya na kwa hakika nchi nzima na ajenda yake inavutia kila mtu," ilisoma.

Walimfananisha na Kamala Harris, makamu wa rais wa Marekani na Rais wa Tanzania Samia Suluhu kwa ukali, ufasaha, akili na ushujaa.

Viongozi hao wa vijana pia waliangazia maendeleo Kirinyaga, Suala la naibu wa Ruto linaonekana kama viazi moto ndani ya Muungano mkubwa wa Kenya Kwanza, kama chaguo la Raila Odinga.

Mgombea mwenza kutoka eneo la Mlima Kenya anatarajiwa kuongeza nafasi zao za ushindi wao.

(Utafsiri: Samuel Maina)