Mbunge Wanyonyi:Niko ODM kukaa

Muhtasari
  • Mbunge huyo, hata hivyo, amekanusha madai hayo kwa kusema falsafa yake ya uongozi imekuwa ikiwahusu watu na itabaki kuwa hivyo

Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi sasa anasema yuko imara katika chama cha ODM na Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance.

Haya yanajiri baada ya mgombea ugavana wa muungano wa Kenya Kwanza Johnson Sakaja kudai kuwa walikuwa kwenye mazungumzo ya kufanya kazi pamoja kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

Katika video aliyoshiriki kwenye Twitter, Wanyonyi alisema kuwa atakuwa akitetea kiti chake cha ubunge.

"Niko tayari kutumikia watu wa Westlands kwa mara ya tatu na ninasalia imara katika chama changu cha ODM na Azimio la Umoja One Kenya. Asanteni kwa wafuasi wangu wote kwa kuniamini, ndoto hiyo inaendelea," alisema.

Hii ni mara ya kwanza kwa Wanyonyi kutangaza msimamo wake wa kisiasa tangu Azimio ilipotoa tikiti yake ya kiti cha ugavana wa Nairobi kwa Polycarp Igathe wa Jubilee.

Baada ya kupigwa kiwiko kwenye kinyang'anyiro cha ugavana, mbunge huyo alianza kutoa ishara tofauti kuhusu mustakabali wake wa kisiasa.

Kupigwa picha akiwa na Sakaja siku alipoachia ngazi na baadaye kutoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilidokeza kuwa alikuwa akifikiria upya mustakabali wake wa kisiasa zilileta mkanganyiko wa aina fulani miongoni mwa wafuasi wake.

Mbunge huyo, hata hivyo, amekanusha madai hayo kwa kusema falsafa yake ya uongozi imekuwa ikiwahusu watu na itabaki kuwa hivyo.

"Uongozi umekuwa wa kutumikia watu. Hii imekuwa falsafa yangu kwa miaka 15 iliyopita na nina imani itabaki kuwa hivyo. Kama nilivyosema hapo awali, haijawahi kunihusu, haitanihusu mimi. daima b kuhusu watu. Si mimi ni sisi."

Akizungumza katika Kituo cha Hustler siku ya Jumatano baada ya kupokea cheti chake cha uteuzi wa chama cha UDA, Sakaja alisema alikutana na mbunge huyo mara kadhaa.