IEBC yatangaza majina ya maafisa watakaosimamia uchaguzi wa Agosti 9

Muhtasari

• Notisi ya gazeti la serikali ya Aprili 28 ilionyesha kuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati atakuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Urais mnamo Agosti 9.  

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imechapisha kwenye gazeti rasmi la serikali majina ya Wasimamizi wa Uchaguzi (ROs) watakaosimamia Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.  

Notisi ya gazeti la serikali ya Aprili 28 ilionyesha kuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati atakuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Urais mnamo Agosti 9.  

Katika ilani hiyo IEBC imewataja Wasimamizi wa Uchaguzi katika maeneo bunge na manaibu wasimamizi wa uchaguzi.  

Msimamizi wa Uchaguzi kwa raia wa Kenya wanaoishi nje ya Nchi atakuwa Abdidahir Maalim na Naibu Msimamizi wa Uchaguzi ni William Tumaini Kahindi.  

"Uteuzi huo ni kwa madhumuni ya zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022," notisi ya gazeti la serikali ilieleza.  

“Wasimamizi wa Uchaguzi wa maeneo bunge na Manaibu Wasimamizi wa Uchaguzi pia watasimamia  zoezi usajili na ukaguzi kwa madhumuni ya uhakiki wa sajili ya wapiga kura zoezi ambalo limepangwa kufanyika kuanzia tarehe 4 Mei, 2022 hadi Juni 2, 2022.  

Majukumu ya Wasimamizi wa Uchaguzi ni kama ifuatavyo:  

 • Kutangaza matokeo ya uchaguzi katika eneo maalum la uchaguzi;  

• Kusaini fomu rasmi za kutangaza matokeo;  

• Kusambaza matokeo rasmi kwa kituo cha kitaifa cha kuhesabia iwapo mfumo wa upokezi wa kielektroniki unatumika;  

• Kupeleka fomu rasmi ya kutangaza matokeo kwa kituo cha kitaifa cha kujumlisha matokeo;  

• Kutangaza mshindi katika eneo fulani la uchaguzi;  

• Kusaini na kutoa cheti rasmi kwa mshindi; 

 • Anasimamia uajiri, mafunzo na kuwapa majukumu maafisa wengine wa uchaguzi; 

• Kutoa uamuzi kuhusu kura zenye utata.