Martha Karua ndiye mgombea mwenza bora -TIFA

Muhtasari

• Utafiti huo unaonyesha kuwa Wakenya zaidi (85%) wanampendelea mgombea mwenza wa Raila Odinga ikilinganishwa na asilimia 59 ambao wanaweza kumtambua Rigathi Gachagua.

Mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua akihutubia wananchi
Mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua akihutubia wananchi
Image: WANGESHI WANGONDU

Mgombea mwenza wa Azimio la Umoja Martha Karua ndiye mgombea mwenza maarufu zaidi kati ya manaibu walioteuliwa wa wagombea watatu wakuu wa kisiasa, utafiti wa Tifa unaonyesha. 

Utafiti huo unaonyesha kuwa Wakenya zaidi (85%) wanampendelea mgombea mwenza wa Raila Odinga ikilinganishwa na asilimia 59 ambao wanaweza kumtambua Rigathi Gachagua kama mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto. 

Utafiti huo unasema asilimia 85 ya wanaoweza kumtaja Karua ni sehemu ya asilimia 90 walioonyesha nia ya kumuunga mkono Raila kuwania urais. Asilimia 59 ambao wanaweza kumtambua Gachagua ni kutoka asilimia 69 ya waliohojiwa ambao walisema wanapendelea Ruto kuwa rais ajaye. 

Mtafiti mkuu Tom Wolf alitumia mifano miwili ambayo inaweza kueleza kwa nini Karua ni maarufu zaidi.

 "Maoni yangu binafsi ni kwamba Karua ni maarufu zaidi kwa sababu amekuwa katika umaarufu wa kisiasa kwa muda mrefu baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka wa 1992. 

"Pili, uangalizi wa vyombo vya habari juu yake umekuwa mkubwa, uzinduzi wake katika KICC ulionekana kama mkutano wa kisiasa ikilinganishwa na uzinduzi wa Gachagua huko Karen," Wolf alisema. 

Kulingana na kura hiyo, asilimia 38 ya waliohojiwa walisema wanamuunga mkono kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuwania urais, lakini walikuwa na ufahamu mdogo sana kuhusu mgombea mwenza wake, Andrew Sunkuli. 

Ni asilimia 21 pekee waliosema wanafahamu kuwa Sunkuli ndiye mgombea mwenza wa Kalonzo. 

"Labda, katika wiki zijazo (kama sio siku) karibu Wakenya wote watakuja kufahamu hawa wagombea-wenza waliotangazwa hivi majuzi ni akina nani," Wolf alisema. 

"Basi itawezekana kufanya tathmini ya kamili zaidi ya athari zao katika nia ya kupiga kura mnamo Agosti," aliongeza. 

Jumla ya wahojiwa 1,719 walishiriki katika kura hii ya maoni ambayo ilifanyika kati ya tarehe 15-16 Mei 2022. 

Utafiti huo, ambao ulikuwa na kiasi cha makosa ya +/- asilimia 2.34, ulifadhiliwa na kampuni ya Utafiti ya Tifa. 

Utafiti wa kitaifa ulifanyika katika kanda tisa; Katika mwa Bonde la Ufa, Pwani, Mashariki ya Chini, Mt Kenya, Nairobi, Kaskazini, Nyanza, Kusini mwa bonde la Ufa na Magharibi. 

Utafiti huo ulionyesha kuwa mrengo wa Azimio ndiyo iliyopendelewa zaidi katika kuchukuwa usukani wa urais huku asilimia 39 ya waliohojiwa wakichagua Azimio ikilinganishwa na asilimia 35 waliopendelea Kenya Kwanza.