Mpigie kura mgombea urais umtakaye- Kiunjuri awaambia wakazi wa Mt Kenya

Muhtasari

•Kiunjuri aliambia wakazi eneo la Mlima Kenya kuzingatia uwezo wa uongozi wa wagombea viti na wala si vyama vyao.

•Mnamo Jumatatu, Kiunjuri aliibua wasiwasi kuhusu kutengwa katika uendeshaji wa masuala katika Muungano wa Kenya Kwanza.

Kiongozi wa TSP Mwangi Kiunjuri wakati wa mkutano na wanahabari katika afisi za TSP mnamo Januari 28, 2022.
Kiongozi wa TSP Mwangi Kiunjuri wakati wa mkutano na wanahabari katika afisi za TSP mnamo Januari 28, 2022.
Image: MERCY MUMO

Huku ikiwa imesalia takriban miezi miwili kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, kiongozi wa The Service Party Mwangi Kiunjuri sasa anataka eneo la Mlima Kenya kumpigia kura mgombea urais yeyote wanayemtaka..

Katika kile kinachozuka kama mzozo katika Muungano wa Kenya Kwanza, Kiunjuri aliambia wakazi eneo la Mlima Kenya kuzingatia uwezo wa uongozi wa wagombea viti na wala si vyama vyao.

"Watu kutoka Kaunti ya Laikipia na eneo la Mlima Kenya, wachagueni viongozi na sio vyama, Mchagueni rais mnayemtaka na mtafute viongozi mtakaowapigia kura, kwa nyadhifa zingine," Kiujuri alisema katika mahojiano na Inooro TV Jumatano jioni.

Matamshi hayo yanapingana na  msimamo wake wa awali ambao amekuwa akionyesha wakati akihutubia umati na hata mikutano ya wanahabari.

Waziri wa Kilimo wa zamani amekuwa akipigia debe azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais.

Chama chake cha TSP  kuwa mwanachama wa Kenya Kwanza kulimaanisha kuwa Kiunjuri angetumia jukwaa la TV kuhimiza eneo la Mlima Kenya kumpigia kura Ruto badala ya kuacha chaguzi wazi kwa wafuasi wake.

Je, inaweza kuwa ni ishara ya kuanguka kwa Muungano wa Kenya Kwana?

Mnamo Jumatatu, Kiunjuri aliibua wasiwasi kuhusu kutengwa katika uendeshaji wa masuala katika Muungano wa Kenya Kwanza.

Kenya Kwanza inajumuisha vyama 14 vya kisiasa, vikiwemo UDA cha Ruto, ANC cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha Moses Wetangula kama washirika wakuu.

Alisema baadhi ya vyama vimefichwa na kupuuzwa katika kutekeleza kampeni, jambo ambalo alionya linaweza kuhatarisha azma ya Ruto ya kuwania kiti hicho cha juu.

Kiunjuri alisema inashinda mantiki kwa wakuu wa muungano kuwafanyia kampeni wagombeaji wanaoegemea vyama vyao lakini muungano huo unakaribia uchaguzi wa Agosti kama umoja.

"Unapokuwa katika muungano, unahitaji kufanya kazi kama timu. Huwezi kujifanya mchana kuwa uko katika muungano na usiku, hauko katika muungano,” Kiunjuri alisema.

“Siwezi kwenda Nyandarua leo na kuwaomba watu wa Nyandarua kuunga mkono mgombeaji wa TSP wakati tuna wagombea wa ANC, Ford Kenya, Tujibebe na CCK. Ningekuwa mnafiki.”

Pia imebainika kuwa kuna dhoruba katika kambi ya Kenya Kwanza huku vyama washirika vikipigania kugawa maeneo na pesa taslimu kwa ajili ya kampeni.