Ruto aondoka nchini kwa safari ya dharura, huku Raila na Kalonzo wakizuru DRC

Muhtasari

• Ruto alipokuwa akiondoka nchini, mkubwa wake Rais Uhuru Kenyatta pia aliondoka kuelekea Mogadishu ambako alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.

Image: DP RUTO/TWITTER

Naibu Rais William Ruto siku ya Alhamisi alikatiza kampeni zake Kaskazini mwa Kenya na kuondoka nchini 'kwa kipindi kifupi.' 

Ruto, hata hivyo, anatarajiwa kurejea nchini siku ya Ijumaa kuhudhuria kongamano la kitaifa la wanawake la Kenya Kwanza litakaloandaliwa katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo. 

Ruto alitarajiwa kufanya kampeni mjini Marsabit na Isiolo siku ya Alhamisi kabla ya kuanza ziara nyingine katika kaunti ya Laikipia siku ya Jumamosi. 

Hata hivyo, ghafla alikatisha kampeni yake ya kisiasa katika eneo hilo na kuondoka nchini kwa shughuli isiyojulikana. 

"Kiongozi aliondoka nchini Alhamisi kwa notisi fupi kwa shughuli ya kibinafsi lakini atarejea Ijumaa," afisa wa ngazi ya juu wa kampeni za Ruto ambaye hana idhini ya kuongea kwa niaba ya Naibu Rais alisema. 

Ruto alipokuwa akiondoka nchini, mkubwa wake Rais Uhuru Kenyatta pia aliondoka kuelekea Mogadishu ambako alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.

Ujumbe wa Uhuru katika nchi jirani ulijumuisha Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa na mwenzake wa Kilimo Peter Munya. 

Ziara ya Ruto nje ya nchi ilijiri siku moja baada ya mpinzani wake mkuu katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 Raila Odinga pia kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumatano asubuhi. 

Raila aliondoka saa chache baada ya Waziri Mkuu mteule wake Kalonzo Musyoka pia kuondoka nchini Jumanne. Kinara huyo wa Wiper inasemekana aliungana na Raila nchini Congo kwa shughuli ambayo haikufahamika maelezo yake. 

Wanatarajiwa kurejea nchini kufikia Jumapili. 

Hii ni mara ya pili kwa Ruto kuondoka nchini mwaka huu. Mnamo Februari 27, Ruto aliondoka nchini kwa safari ya siku 12 iliyompeleka Marekani na Uingereza. 

Safari hiyo rasmi ilitangazwa sana huku Naibu Rais akitumia fursa hiyo kukashifu serikali ya Rais Uhuru Kenyatta. 

Alishutumu utawala wa Jubilee kwa kuteka nyara taasisi za serikali na kuzitumia kama silaha katika vita dhidi ya ufisadi. Ruto alizungumza na makundi ya wataalam wa kisiasa na kiuchumi nchini Marekani na Uingereza akielezea ajenda yake kwa nchi na kuahidi mapinduzi ya kiuchumi iwapo atachaguliwa kuwa rais.