Ni wazi kuwa kinyang'anyiro cha urais Agosti ni cha farasi 3-Kabogo asema

Muhtasari
  • Kabogo alisema uungwaji mkono wa Wajackoyah kote kanda ya kati unaanza kuimarika na hauwezi kupuuzwa
WILLIAM KABOGO
Image: WILLIAM KABOGO/TWITTER

Mgombea Ugavana wa Kiambu William Kabogo anasema kuingia kwa kiongozi wa Roots Party Prof. George Wajackoyah katika kinyang'anyiro cha Agosti hadi Ikulu kumebadilisha mienendo ya kile kilichoitwa MBio za farasi wawili.

Kulingana na Kabogo ambaye ni kiongozi wa chama cha Tujibebe Wakenya, Prof. Wajackoyah ni ‘farasi’ wa tatu pamoja na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio La Umoja Raila Odinga katika azma ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

"Wiki moja ni kama miaka kumi katika siasa. Tunaona mabadiliko mengi uchaguzi unapokaribia. Hapo awali, farasi walikuwa wawili lakini sasa huwezi kusema ni mbio za farasi wawili,” Kabogo alisema katika mahojiano na NTV Jumatatu.

"Kwa sasa tunaangalia farasi watatu."

Kabogo alisema uungwaji mkono wa Wajackoyah kote kanda ya kati unaanza kuimarika na hauwezi kupuuzwa.

“Nilikuwa nikifanya kampeni Kiambu na naweza kusema kuna watu ambao watampigia kura Raila, wengine Ruto na sasa Wajackoyah. Kwa kutajwa tu kwa jina lake, unaweza kuhisi kitu katika umati wa watu, na huwezi kulifumbia macho hilo, "aliongeza.

Jitihada za Wajackoyah zimekuwa zikifurahia umaarufu mkubwa miongoni mwa wapiga kura vijana kote nchini, kutokana na mpango wake wa kuhalalisha bangi iwapo atashinda urais.