Pauline Njoroge: Niliwahi kuwa na wazo na kununua digrii kwa 100K

Muhtasari

• Mwanablogu wa Azimio la Umoja alieleza kwamba baada ya kukosa namna ya kuendeleza masomo yake ya chuo kikuu, alijiwa na wazo la kughushi digrii kwa kiasi cha laki moja.

Pauline Njoroge
Image: Facebook

Mwanablogu maarufu wa muungano wa Azimio la Umoja Pauline Njoroge ameelezea kumbukumbu nzito jinsi alijipata katika shinikizo kali la kutaka kununua digrii ili kupata kazi baada ya kuahirisha masomo yake ya chuo kikuu kutokana na uhaba wa pesa za kugharamia masomo hayo.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Njoroge alielezea kwamba mnamo mwaka 2014, alijiwa na wazo la kutaka kununua shahada baada ya kuachia masomo njiani kutokana na kwamba hangeweza kufadhili masomo ya dadake mdogo na kujifadhili pia, jambo lililomfanya kuahirisha masomo yake hadi pale ambapo mdogo wake atakapomaliza chuo.

Wazo la kutaka kughushi digirii lilimjia pale alipogundua kwamba huenda atapoteza nafasi nyingi za kupata kazi na kwamba hakuwa anaona matumaini mbele hata kidogo – alikuwa katika kiza kinene na kuwa na digrii tu ndilo hakikisho tosha la kupata kazi.

Hapo ndipo alifikiria na kujiambia kwamba angehangaika na kuweka kibindoni laki moja taslimu pesa za Kenya katika kununua shahada ili kujaribu bahati yake katika soko la kutafuta kazi.

"Kwa kuona hakuna mwanga mbele na kujua kwamba ningekosa fursa kwa sababu ya ukosefu wa karatasi, nilifikiri njia rahisi zaidi ilikuwa kuweka kibindoni 100k na kununua kwa taasisi ambayo ingeghushi cheti kwa ajili yangu. Kusema ukweli, sikujua hata bei ya soko kwa hiyo nilikuwa nakisia tu" aliandika Njoroge.

Mipango yake hiyo ilipata pigo baada ya kumuelezea Rafiki yake mmoja ambaye alimuapiza na kumkemea vikali huku akimtaka apotezee fikira hizo mara moja na badala yake kuweka tumaini lake kwa Mungu.

Baada ya kulikabidhi suala lake kwa Mungu, pakatokea mtu akampa fedha kiasi za kujiunga chuo kikuu tena na hapo ndipo safari yake ya mafanikio kimasomo ilipoanza kwani kufikia mwaka 2017 alifanikiwa kupata kazi ya mawasiliano katika kampuni moja ambapo bado alikuwa anaendelea na masomo ya shahada yake ya kwanza huku mwenye kazi alikuwa anatafuta mtu mwenye shahada ya uzamili lakini kwake ikawa ni bahati kwa sababu kigezo walikuwa wanakitafuta kwa mfanyikazi alikuwa nacho hata bila digirii.

Hapo vilevile wazo la kughushi digrii lilimuandama kwani hakuwa anataka kupoteza ile kazi kizembe kwa kukosa digirii, lakini alijikaza kupotezea wazo hilo.

Hatimaye mwaka 2018 Pauline Njoroge alihafili nac digrii yake ya kwanza na mwezi mmoja baadae akajiunga na chuo kikuu cha kimataifa kufanya digrii ya uzamili.

Miaka miwili baadae alipata kazi nzuri katika shirika la umoja wa Afrika AU, wakati ambapo alikuwa anahafili digrii ya uzamili.

Njoroge ameibua simulizi hii kuhusu safari yake ya masomo ya chuo kikuu kipindi ambapo Johnson Sakaja wa mrengo wa Kenya Kwanza anaandamwa na madai ya kughushi digrii kutoka chuo kimoja nchini Uganda, TEAM.