Ulipewa kazi, umefanya nini?- Rais Kenyatta amshambulia Ruto

Muhtasari

•Uhuru alisema Ruto  alikuwa na miaka minane ya kutekeleza ahadi nyingi za maendeleo anazotoa sasa lakini hakuweza.

•Rais aliwahimiza Wakenya kufanya maamuzi ya busara kabla ya uchaguzi wa Agosti huku akiwakumbusha mustakabali wao uko hatarini.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta bado ameendelea kumtupia vijembe naibu wake William Ruto huku zikiwa zimesalia siku 38 tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika KICC Jumamosi, Rais bila kutaja jina lake, alimsuta naibu wake kwa kutoa ahadi nyingi ilhali alikuwa na fursa ya kutekeleza.

Uhuru alisema DP alikuwa na miaka minane ya kutekeleza ahadi nyingi za maendeleo anazotoa sasa lakini hakuweza.

"Nasikitika nikiona wengine huko ng'we ng'we. Mtu amepewa kazi, badala ya kazi ni mdomo, mdomo, mdomo tu. Alafu anaanza kusema tutafanya na tutafanya," alisema.

"Kwa nini haukufanya ukiwa na kazi.Hii maneno ya makelele huko, huko, watu wawache upuzi... Munya hapa amefanya kazi kwa miaka mitatu. Hao walikua miaka nane walifanya nini?"

Aliongeza:

"Wakiona mtu na shida wanasema watatatua. Kwa nini hamkutatua mkiwa ofisini?"

Rais aliendelea kuwahimiza Wakenya kufanya maamuzi ya busara kabla ya uchaguzi wa Agosti huku akiwakumbusha mustakabali wao uko hatarini.

Uhuru alibainisha kuwa hajashurutisha mtu yeyote kuunga mkono kambi fulani lakini akasema ni juu ya Wakenya kutathmini viongozi wao kabla ya kuwapigia kura.

"Lakini vile nimesema ni shauri zenu. Sijalazimisha mtu kitu nimesema mfikirie. Fikira, Fikiria, Fikiria."