Mdahalo wa ugavana Nairobi: Sakaja amkashifu Igathe kwa kugura ofisi na kumtema Sonko

Sakaja alionya kwamba ikiwa wenyeji wa Nairobi watachagua Igathe huenda akawaacha tena.

Muhtasari

•Sakaja alidai kuwa Mike Sonko huenda hangetimuliwa kama Igathe ambaye alikuwa naibu wake alisalia ofisini. 

•Sakaja alisema kuondoka mapema kwa Igathe ni suala la uadilifu na anapaswa kulaumiwa kwa matokeo yake.

Wagombea ugavana wa Nairobi Johnston Sakaja na Polycarp Igathe

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja Jumatatu alimkashifu mpinzani wake Polycarp Igathe kwa kuondoka ofisini mapema 2018.

Alidai kuwa gavana wa zamani Mike Sonko huenda hangetimuliwa kama Igathe ambaye alikuwa naibu wake alisalia ofisini. 

Sakaja alizungumza wakati wa mdahalo wa gavana wa Nairobi katika Chuo Kikuu cha Catholic University of Eastern Africa huko Karen.

"Gavana Sonko hangevuliwa mamlaka ikiwa ungekwama afisini. Kwa hakika ikiwa ungekwama afisini, huenda sasa ungekuwa gavana aliye madarakani. Hakungekuwa na fujo Nairobi," alisema.

Sakaja aliongeza kuwa chanzo cha baadhi ya matatizo yanayoukabili Mji Mkuu ni hatua ya kuondoka kwa Igathe.

Mwaniaji huyo wa ugavana alionya kwamba ikiwa wenyeji wa Nairobi watachagua Igathe mnamo Agosti 9, anaweza kuwaacha tena pindi akikabiliwa na msukumo  mkubwa

Sakaja alisema kuondoka mapema kwa Igathe ni suala la uadilifu na anapaswa kulaumiwa kwa matokeo yake.

"Uadilifu hufafanua kiongozi sio tu hadharani lakini pia kwa faragha. Uadilifu sio kuwa mkamilifu; ni kuhusu kuwajibika," aliongeza.

Kwa upande wake, Igathe alijitetea akisema wapiga kura wanapaswa kuzingatia siku zijazo, na kuongeza kuwa ataboresha maisha yao ikiwa watamchagua.

"Nataka niwahakikishie, Nairobi itakuwa kitu cha ndoto zako, itakuwa jiji la maono yako," alisema.

Igathe aliondoka ofisini ghafla mwezi Januari 2018 akilalamikia ukosefu wa uaminifu kati yake na Sonko.

"Imekuwa furaha kubwa kuwahudumia wakazi wa Nairobi na nitaendelea kuhudumu kama mshauri, zaidi ya nafasi yangu ya awali ya naibu gavana wa kaunti ya Nairobi," alitangaza kwenye Twitter huku akiaga afisi ya naibu gavana.