Mimi sio mradi wa seikali,mimi ni mradi wa wananchi-Wajackoyah

Wajackoyah alisema kuwa anapuuzwa kwa sababu wapinzani wake wanafikiri yeye si mtu.

Muhtasari
  • Wajackoyah alisema kuwa anapuuzwa kwa sababu wapinzani wake wanafikiri yeye si mtu
  • Mgombea huyo wa urais alishutumu miungano hiyo miwili kwa kumpuuza bila kufanya juhudi zozote kujua anachofanyia jamii
Mgombea urais Wajackoyah,wakati wa mahojiano na Radiojambo 10/juni/2022
Image: CHARLENE MALWA

Mgombea urais wa chama cha Roots George Wajackoyah amemshutumu mwaniaji urais wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kwa kuwa mradi wa serikali.

Akizungumza katika KTN News Jumapili, Wajackoyah alipuuza madai kwamba yeye ni mradi wa serikali na zaidi akamshutumu mwenzake wa Kenya Kwanza William Ruto kuwa mradi wa serikali.

“Kwanza Raila Odinga ni mradi wa serikali, Ruto mwenyewe ni mradi ndani ya mradi fulani serikalini, mimi niko hapa mimi ni mradi wa wananchi,” Wajackoyah alidai.

Wajackoyah alisema kuwa anapuuzwa kwa sababu wapinzani wake wanafikiri yeye si mtu.

"Kuna shida katika nchi hii. Kuna shida ya Ruto na wenzake na pia kuna shida ya Raila na wenzake. Nilitoka popote, walinidharau kabisa jinsi Barack Obama alivyopuuzwa," alisema. .

Mgombea huyo wa urais alishutumu miungano hiyo miwili kwa kumpuuza bila kufanya juhudi zozote kujua anachofanyia jamii.

"Nikifanya jambo ambalo halimpendezi Azimio au Ruto unaona watu wakija na kutweet. Nikizungumza kuhusu jambo ambalo linapendelea upande mmoja utalalamika," alisema Wajackoya.

Aliongeza kuwa madai kama hayo yanapotolewa inaonyesha kuwa kambi zingine zimehisi kushindwa.