Hili litakuwa jaribio langu la mwisho la urais- Raila atangaza

Raila amesema uchaguzi mkuu wa mwaka huu ndio utakuwa wake wa mwisho kuwania urais

Muhtasari

•Raila alisema hana nia ya kugombea tena kwa sababu ya umri wake lakini bado atakuwa na mengi ya kufanya nje ya siasa.

•Mwezi uliopita, kiongozi huyo wa ODM alisema atakubali kushindwa iwapo atapoteza katika uchaguzi wa Agosti 9. 

Kinara wa ODM Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga amesema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ndio utakuwa wake wa mwisho kuwania urais. 

Alisema hana nia ya kugombea tena kwa sababu ya umri wake lakini bado atakuwa na mengi ya kufanya nje ya siasa za uchaguzi. 

"Nimekuwa nje ya siasa kali lakini Umoja wa Afrika uliniteua kama Mwakilishi Mkuu wa miundombinu na ilinifanya kuwa bize," Raila alisema katika mahojiano na BBC.

Waziri huyo mkuu wa zamani ambaye ana umri wa miaka 77 aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka wa 1997 na kushindwa na aliyekuwa rais marehemu Daniel Moi.

Mwaka wa 2007 aliwania tena na kushindwa na Mwai Kibaki , 2013 na 2017 alishindwa na Rais Uhuru Kenyatta. 

Mwezi uliopita, kiongozi huyo wa ODM alisema atakubali kushindwa iwapo atapoteza katika uchaguzi wa Agosti 9. 

Raila, ambaye atakuwa anawania urais kwa mara ya tano anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Naibu Rais William Ruto wa UDA. 

Kiongozi huyo wa ODM ambaye amekuwa akizunguka nchi nzima katika juhudi za kusaka kura ameahidi kutoa malipo ya kila mwezi ya Sh6,000 kwa familia maskini. 

Pia ameahidi kuanzisha bima ya afya ya Baba Care ili kuwasaidia Wakenya.  

Kulingana na manifesto ya Azimio, Raila anapanga kufanya viwanda kama kichochezi cha mapinduzi ya kiuchumi ya serikali ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kusababisha ajira na uzalishaji mali.

Pia zitasaidia ukuaji wa MSMEs, ikijumuisha sekta ya JuaKali kupitia uboreshaji wa tija na ufanisi.