Mwanariadha Ezekiel Kemboi amuidhinisha Raila kuwa rais

"Mi nimekuja hapa kama last born wa Baba. Kwa majina naitwa Ezekiel Kemboi Amolo," alisema

Muhtasari

•Mwanariadha huyo alipokuwa akiwahutubia wakazi alisema Raila ndiye chaguo bora zaidi kwa eneo hilo.

•Alibainisha kuwa uwepo wake katika timu ya Raila ulimaanisha kuwa masuala ya vijana yatapewa kipaumbele

Kinara wa ODM Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Bingwa wa dunia mara tatu Ezekiel Kemboi amemuidhinisha mgombea urais wa Azimio Raila Odinga kuchukua kiti hicho cha juu..

Alizungumza Jumapili wakati wa kampeni za Muungano huo mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Mwanariadha huyo alipokuwa akiwahutubia wakazi alisema Raila ndiye chaguo bora zaidi kwa eneo hilo.

"Mi nimekuja hapa kama last born wa Baba. Kwa majina naitwa Ezekiel Kemboi Amolo," alisema.

Mwanariadha huyo alibainisha kuwa uwepo wake katika timu ya Raila ulimaanisha kuwa masuala ya vijana yatapewa kipaumbele

"Mkiona niko hapa, maswala ya vijana nitashughulikia. Hamtakuwa mnapiga simu. Mimi mwenyewe nitakuwa nyumbani. Mi nitawakaribisha nyumbani."

Raila alikuwa amepeleka kampeni zake hadi nyumbani kwa kiongozi wa UDA William Ruto, ambapo aliongoza safari kutoka kaunti ya Nandi hadi Uasin Gishu.

Akizungumza wakati wa kampeni, Junet aliahidi kuwa utawala wa Azimio utashughulikia mahitaji ya wakulima.

Mgombea mwenza wa Raila Martha Karua alisema wana nia ya kuhimiza usawa kwa Wakenya wote bila kujali itikadi za kisiasa, tabaka au jinsia.

Aliwataka wapinzani wao kuacha kusema uwongo kwamba maisha yao yako hatarini ilhali wanafurahia ulinzi wa serikali.

"Ninamsihi DP, Iwapo unafikiri kuna mtu yeyote katika kaya yako yuko hatarini, tafadhali wape maafisa. Na kama maafisa hawatoshi, umeajiriwa na Serikali, omba maafisa zaidi," alisema.

"Lakini nakuomba, tafadhali usiliongoze taifa letu kwenye mwelekeo mbaya, ukisema mambo unayojua si ya kweli kama kwamba familia yako iko hatarini."

Haya yanajiri baada ya Ruto kudai kuwa bosi wake Rais Uhuru Kenyatta alikuwa akimtishia, na kumtaka kuwaepusha watoto wake.

“Kwa heshima kubwa uwe binadamu mwenye heshima, sisi ndio tulikusaidia hivyo acha kujifanya sasa hivi, umeanza kunitisha lakini ilimradi usiwadhuru watoto wangu, tuheshimiane,” alisema. alipokuwa akizungumza huko Kapsabet, Kaunti ya Nandi siku ya Ijumaa.

Karua alishangaa jinsi wananchi watakavyojisikia salama ikiwa mtu katika nafasi ya Ruto anahisi kutishiwa.

"Hakuna matumizi ya kusema uwongo kwa sababu za kisiasa. Inabidi tukubaliane kuhusu kile ambacho Wakenya hawa wataamua Agosti 9," alisema.

Kiongozi huyo wa Narc alikariri wito wake kwa Wakenya kuwapigia kura viongozi waadilifu, wanaokumbatia uadilifu.