Uchaguzi 2022: Vigogo wa siasa kidete kutetea azma yao huku Agosti 9 ikizidi kubisha hodi

Kwa sasa, Ruto na Odinga wameelekeza kampenzi kwenye ngome zao.

Muhtasari

•Raila na Ruto wanajijengea sifa lukuki kwa yale ambayo wamefanikisha  huku wakielekeza lawama kwa wapinzani wao.

•Kila mwanasiasa yuko tayari kufanya jambo lolote kumbamiza mpinzani wake almradi aibuke mshindi.

wakati wa kampeni huko Nandi Hills, Kaunti ya Nandi mnamo Jumatatu, Julai 25,2022.
Naibu Naibu Rais William Ruto wakati wa kampeni huko Nandi Hills, Kaunti ya Nandi mnamo Jumatatu, Julai 25,2022.
Image: FACEBOOK// WILLIAM RUTO

Huku zikiwa zimesalia siku saba kwa uchaguzi mkuu kufanyika, kila mgombea yuko mbioni kusaka kura katika maeneo yenye asilimia kubwa ya wapiga kura.

Maswala ibuka katika kampeni  hizi ni ikiwemo  utendakazi  na uadilifu wa maafisa wa serikali na wanasiasa walioshamiri ahadi si haba huku wakitaka uungwaji mkono ili kuibuka washindi katika kinya'nga'nyiro cha  wiki ijao.

Cheche na kauli mbalimbali bado  ni hali inayozonga siasa na kampeni za uchaguzi.

Kila mwanasiasa yuko tayari kufanya lolote kumbamiza mpinzani wake almradi aibuke mshindi.Hii ni njia mojawapo wanayotumia ili kuwapumbaza raia ambao asilimia kubwa wameathirika kwa namna moja au nyingine na kwa mara hupiga kura kwa misingi ya kikabila.

Wiki jana, kiongozi wa United Democratic Alliance[UDA] na ambaye ni  mgombea kiti cha urais kupitia  muungano wa Kenya Kwanza,  William Ruto, alitoa madai kwamba familia yake imo hatarini kwa kile ambacho alikitaja  kuwa “Vitisho”.

Bwana Ruto akiuza sera zake  katika kaunti ya Nandi, alitilia shaka hatua ya serikali kuwalazimisha  machifu na maafisa wengine serikalini kupigia kampeni mpizani wake  wa Azimio la umoja one-Kenya Raila Odinga. Alisema kwamba atawapandisha vyeo ikiwa atashinda kura.

“ Machifu wanaolazimishwa kupigia kampeni bwana kitendawili ama hata tayari wengine wamefutwa, nitawarudisha kazini na kuwapandisha cheo. Serikali yangu itatambua kazi yenu na kuwapa nafasi kutumikia kitaalam hawa wananchi,”Alisema Ruto.

Kwa upande wake Bwana Odinga, akiwa katika kaunti ya Machakos, alimshauri Ruto kutafuta mgombea mwenza mwingine maana mbunge wa Maathira Rigathi Gachagua amehusishwa na ufisadi na kulingana na katiba, mtu yeyote aliyehusishwa na sakata au maadili na utendakazi wake ni wa kutiliwa shaka, basi hastahili kuwania au kushikilia nafasi yoyote ya uongozi.

Kinachoonekana kati ya wanasiasa hawa, ni kwamba wanajijengea sifa lukuki kwa yale ambayo wamefanikisha  huku wakielekeza lawama kwa wapinzani wao.

Ruto anasema yuko tayari kufanya mabadiliko makubwa  ikiwa atachaguliwa kuwa rais.

 Lawama anaielaekeza kwa handisheki baina ya Rais Uhuru na Bw Odinga akidai kwamba ndiyo iliyosambaratisha mpango wa “big four agenda” pamoja na madhila kama vile mfumuko wa bei za bidhaa ambayo imefanya maisha wa wachochole kuwa mbaya zaidi.

Odinga anapigia upato vita dhidi ya ufisadi na  uboreshaji wa maisha ya wakenya kupitia mradi wa 'Babacare'. Atakuwa akiipigia debe sera hii yake katika kipindi kilicho salia.

Katika kampeni na mdahalo wa wangombea kiti nyadhifa mbalimbali, hili swala la ufisadi limekuwa mada ya mazungumzo.

Kila mmoja ameonekana kukubaliana kwamba  matumizi mabaya ya mali ya umma, umekuwa kidondandugu katika maendeleo ya mkenya.

Ripoti zaonyesha kwamba kwa siku, taifa linapoteza zaidi ya  bilioni mbili[2B] na kwa mwaka  ni takribani billioni laki nane za ushuru. Hapa pesa zinazopotea kutoka KEMSA,taasisi na idara za serikali hazija jumuishwa.

Kwa muda mrefu siasa za Kenya zimeamuriwa na  wingi wa wapiga kura anakotoka mgombea kiti. Hii pia ni sawa na kusema ni sehemu ambako mgombea huyo atapata asilimia kubwa ya kura ilkilinganishwa na maeneo au wapinzani wake.

Kwa sasa, Ruto na Odinga wameelekeza kampenzi  kwenye ngome zao. Raila kwa upande mmoja  anazuru maeneo ya Nyanza na Ruto  bonde la ufa.

Kuna kiwewe kwa wapinzani hawa wakuu ambapo kuna maeneo ambayo tayari wamezuru mara kadhaa kwa minajili ya kuwinda kura .

Maeneo kama vile Mlima Kenya, Pwani na Magharibi . Wachanganuzi wa kiasias wanasema haya ndo maeneo ambayo vigogo hawa wawili watakwaruzana sana maana yamegawanyika sasa na kila mmoja ana tumaini ya kujizolea asilimia nzuri.

Mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio inatumia vigogo au wasemaji wa  jamii ili kuwasawishi wapiga kura  wa jamii zao kupigia kura mrengo fulani. Aliyekuwa spika wa bunge, Francis Ole Kaparo, katibu mkuu wa chama cha wafanyikazi[COTU], Francis Atwoli, wazee wa Njuri  Cheke ambao walimtawaza Raila kugombea kiti cha urais, pamoja n wengine wengi.

Hizi ni siku ambazo mwanasiasa atawakodi wapiga kura kwa madhumini ya kuwa kidedea matokeo yatakapo tangazwa. Wakenya wengi hawamudu maisha yao.

Cha msingi zaidi ni zile ahadi wanazowapa wakazi katika maeneo mbalimbali. Wanasiasa ni werevu katika kusema yale yanayowasibu  jamii fulani na kutoa ahadi kwamba ikiwa watateuliwa, watatatua hayo matatizo. Kwa mfano,migogoro ya mashamba, hali ngumu ya maisha, uhaba wa maji, na utovu wa usalama miongoni mwa zingine.

Wakenya wasikubali kupotoshwa au kuzua vurugu kutona na tofauti za kisiasa kama anavyosema Askofu Ole Sapit. Kura ni njia  ni fursa aliyo nayo mpiga kura kumteua kiongozi ambaye anaona atatimiza matakwa yao.

Piga kura kwa amani, zingatia sera za mwanasiasa ambazo zinafaa kuwa ya kuleta maendeleo enadelevu kwa faida ya jamii yote.