Sihitaji machifu kushinda uchaguzi huu - Raila amkemea Ruto

Aidha alimwambia kiongozi huyo wa UDA kuwa anashindana naye.

Muhtasari
  • Kambi inayoongozwa na Ruto imekuwa ikimshtumu Rais na timu ya Azimio kwa kutumia machifu kuiba kura
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga amemjibu mpinzani wake wa Kenya Kwanza William Ruto kwa madai kuwa Muungano huo ulikuwa ukitumia machifu kuhujumu uchaguzi wa Jumanne.

Akizungumza mjini Kisumu ambako Muungano huo ulifanya mkutano mkubwa siku ya Alhamisi, Raila alimtetea Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ndiye mhusika wa lawama hizo.

“Kusema Uhuru anataka kuvuruga uchaguzi kwa kutumia machifu au kuna vitisho kwa IEBC. Hakuna kitu kama hiyo,"Aliongea Raila.

"Hatuhitaji machifu, wasaidizi wa machifu au utawala ili kushinda uchaguzi huu. Tutashinda kupitia kura za watu wa Kenya."

Alieleza imani yake kuwa Wakenya watampigia kura.

Raila alisema Ruto anafaa kumwacha Uhuru akikiri kwamba anafaa kustaafu kwa amani.

Aidha alimwambia kiongozi huyo wa UDA kuwa anashindana naye.

"Nimewaambia watu wanaotupinga kuwa Uhuru ndiye Rais anayemaliza muda wake wa Jamhuri ya Kenya, mwacheni aende astaafu kwa amani."

"Ikiwa una tatizo, wakabili Raila Odinga na Martha Karua sawa," aliongeza.

Kambi inayoongozwa na Ruto imekuwa ikimshtumu Rais na timu ya Azimio kwa kutumia machifu kuiba kura.

"Makamishna wa Kaunti, Makamishna Wasaidizi wa Kaunti wanalazimishwa kwa vitisho na uwongo kwamba watapoteza kazi zao ikiwa hawatakuwa watendaji wa Azimio," Ruto alidai Alhamisi.

Aidha alidai kuwa kulikuwa na mikutano ya usiku ili kumfanyia hujuma.