Karatasi za Uchaguzi wa Ugavana Kirinyaga Zapatikana Mumias Kakamega

IEBC inaendelea na heka heka za kusambaza vifaa vya uchaguzi katika maeneo mengi nchini mbele ya uchaguzi mkuu Jumanne

Muhtasari

• Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika kaunti ya Kakamega Joseph Ayatta alidhibitisha kisa hicho

Maafisa wa polisi wakikagua kundi la kwanza la karatasi za kupigia kura wakichukua maelezo ya kundi la kwanza la karatasi za kupigia kura za urais katika JKIA mnamo Julai 27, 2022.
Maafisa wa polisi wakikagua kundi la kwanza la karatasi za kupigia kura wakichukua maelezo ya kundi la kwanza la karatasi za kupigia kura za urais katika JKIA mnamo Julai 27, 2022.
Image: THE STAR//ANDREW KASUKU

Usambazaji wa nyenzo za uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Jumanne, Agosti 9, umepamba moto huku tume hiyo ikikimbizana na muda kuhakikisha vifaa hivyo vinafika katika kila kituo cha kupiga kura maeneo yote nchini mbele ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kung’oa nanga chini ya saa kumi na mbili zijazo.

Hata hivyo, mchakato huo umeripotiwa kukumbwa na matukio ya kustaajabisha katika maeneo mbali mbali huku vifaa vilivyokusudiwa kupelekwa maeneo fulani vikipatikana kupelekwa katika sehemu tofauti mbali na sehemu vilivyokusudiwa kutumika kwa uchaguzi mnamo Jumanne Agosti 9.

Karatasi za kupigia kura za Kaunti ya Kirinyaga zilipatikana asubuhi ya Jumatatu katika kaunti ya Kakamega eneo la Mumias Mashariki katika kile kilichosemekana kama ni mchanganyiko wakati wa kupakiwa kwa vifaa hivyo baada ya kuchapishwa.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika kaunti ya Kakamega Joseph Ayatta alidhibitisha kisa hicho na kusema kwamba mipango Madhubuti imewekwa ili kuhakikisha vifaa vilivyofaa kupelekwa sehemu hiyo vinapelekwa mbele ya uchaguzi mkuu na hivyo vya Kirinyaga kurudishwa kwa sehemu husika.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya mkanganyiko kama huo kuonekana kweney kaunti ya Mombasa ambapo vifaa vya kupiga kura za ugavana vilivyokusudiwa kuenda kaunti ya Kilifi vilipatikana vimeenda katika eneo bunge la Mvita kaunti ya Mombasa kimakosa.

Mapema jumatatu pia kuliripotiwa kuwa vifaa vya uchaguzi viliharibiwa katika kaunti ndogo ya Chuka na wananchi waliokuwa na ghadhabu huku kiini cha tukio hilo kikiwa bado hakijabainishwa.

Uchaguzi wa kesho utashuhudiwa kivumbi kikali katika maeneo mbalimbali nchini wananchi wakifanya maamuzi ya kuwasalimisha au kuwatumbukiza kwenye mateso kwa muda wa miaka mitano ijayo.