Ni wakati wa kusonga mbele! Mbunge mkongwe Naomi Shaban akubali kushindwa

Naomi alimpongeza mshindani wake Bwire Okano wa chama cha Wiper.

Muhtasari

•Shaban ambaye alikuwa anatazamia kuchaguliwa kwa muhula wa tano alichukua hatua hiyo Jumanne jioni kupitia simu.

• Naomi ambaye amehudumu kwa miaka 20 aliwaambia wafuasi wake kwamba matokeo ya awali yalionyesha kwamba hatanyakua kiti hicho.

Mbunge wa Taveta Naomi Shaban
Image: DOUGLAS OKIDY

Mbunge wa Taveta Naomi Shaban ambaye amekuwa akihudumu kwa muda mrefu amekubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha mwaka huu.

Shaban ambaye alikuwa anatazamia kuchaguliwa kwa muhula wa tano alichukua hatua hiyo Jumanne jioni kupitia simu.

Naomi, katika kundi la Whatsapp aliwaambia wafuasi wake kwamba matokeo ya awali yalionyesha kwamba hatanyakua kiti hicho.

Naomi ambaye alijiunga na siasa mwaka wa 2002 ni mmoja wa wabunge waliokaa muda mrefu zaidi eneo la Pwani. Amehudumu kama mbunge kwa miaka 20 baada ya kumng'oa aliyekuwa mbunge Basil Criticos.

Alimpongeza mshindani wake Bwire Okano wa chama cha Wiper.

"Watu wema, kuna wakati wa kila kitu. Well done team Bwire," Naibu Kiongozi wa Chama cha Jubilee alisema.

Wanasiasa hao wakongwe walisema wakati umefika wa kuhamia mambo mengine. Aliwapongeza wafuasi wake kwa kumchagua kwa mihula minne.

"Asante kwa kunipa nafasi ya kukuhudumia kwa miaka 20. Ndugu yangu mdogo Okano, nakupongeza," aliandika.

Wawaniaji wengine Moris Mutiso wa ODM pia alikubali kushindwa, na kuahidi wafuasi wake kuendeleza mapambano makubwa wakati ujao.

Mutiso ambaye alipoteza kiti kwa Shaban katika uchaguzi wa 2017 alisema dalili zote ni wazi kuwa ameshindwa.

"Tumepoteza uchaguzi huu, nilikubali nikiwa nimeinua kichwa. Tunaishi kupigana siku nyingine. Turudi kazini sasa," Mutiso alisema.

Kiti hicho kilileta ushindani mkali kutoka kwa wagombea watano; Shaban, Mutiso, Okano, Gaudenzio Muutu (Huru) na aliyekuwa rais wa vijana Didas Mzirai.

Ingawa matokeo rasmi bado hayajatangazwa, matokeo ya awali yaliyoonekana na Star kutoka sehemu ya kituo cha kupigia kura yalionyesha kuwa Okano anaongoza katika kinyang'anyiro hicho.Kwa mfano, katika Ukumbi wa Danida Social, Okano alipata kura 123 huku Shaban akipata kura 94. Mutiso, Gaudenzio na Mzirai walipata kura 7, 2 na 3 mtawalia.

Katika Shule ya Kitoghoto Nursery, Okano alipata 230 dhidi ya 50 za Shaban. Mutiso alipata kura 15 huku Gaudenzio akipata kura moja pekee.

Kuna wapiga kura 41,031 waliosajiliwa katika eneo bunge hilo, wote wamesambaa katika vituo 89 vya kupigia kura kulingana na IEBC.