Rashid Echesa ashambulia mwanahabari katika kituo cha kupigia kura Kakamega

Mwanahabari huyo wa kike aliripotiwa kunyanyaswa baada ya kupiga picha za vijana wakigawana pesa

Muhtasari

•Waziri huyo wa zamani anasemekana kumkabili mwanahabari huyo, akitaka kujua yeye ni nani na kwa nini alikuwa akipiga picha.

•Mwanahabari huyo wa kike aliripotiwa kunyanyaswa baada ya kupiga picha za vijana wakigawana pesa. 

Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Aliyekuwa waziri wa Michezo Rashid Echesa
Image: MERCY MUMO

Aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa amenaswa tena katika sakata huku sasa akidaiwa   kushambulia mwandishi wa habari.

Echesa ambaye anawania ubunge wa Mumias West kwa tiketi ya UDA anaripotiwa kushambulia mwanahabari wa Nation ambaye alikuwa akipiga picha katika kituo cha kupiga kura cha Mumias Township.

Mwanahabari huyo wa kike aliripotiwa kunyanyaswa baada ya kupiga picha za vijana wakigawana pesa. Chanzo cha pesa hizo bado hakijajulikana.

Waziri huyo wa zamani anasemekana kumkabili mwanahabari huyo, akitaka kujua yeye ni nani na kwa nini alikuwa akipiga picha.

Echesa kisha alimsukuma mbele na nyuma, na baadaye kumlazimisha kufuta picha hizo, ambazo baadhi zilikuwa  za mwanasiasa huyo katika kituo cha kupigia kura.

Baada ya shambulio hilo Echesa na walinzi wake wanaripotiwa kuondoka katika kituo hicho kutumia gari ambalo halikuwa na nambari ya usajili.

Mwanahabari huyo aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Mumias na kuarifu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.