Wapiga kura kituo cha Moi Avenue wazua vurugu kwa kucheleweshwa kwa shughuli hiyo

Uwepo wa maafisa kwenye lango haukuwazuia kuingia kwa nguvu.

Muhtasari

• Wapiga kura wengi walikatishwa tamaa na ucheleweshaji na ukosefu wa mawasiliano kutoka kwa wafanyikazi wa IEBC.

Wapiga kura wakivamia lango la Moi avenue.
Wapiga kura wakivamia lango la Moi avenue.
Image: SUSAN MUHINDI

Asubuhi hii ya Jumanne Agosti 9 ni siku ya muhimu sana kwa Wakenya huku taifa likielekea katika debe kuwachagua viongozi wao katika nyadhifa mbalimbali kuwahudumia kwa miaka mitano ijayo.

Katika vituo mbalimbali, watu wamefurika wakiwa ange na ari ya kuwachagua viongozi wao kabla hakujapambazuka.

Jijini Nairobi katika kituo cha kupiga kura cha barabara ya Moi katikati mwa jiji kuu la Kenya, wapiga kura waliojawa na ghadhabu walijitoma katika kituo hicho kwa kile walilalamika kuwa maafisa ya IEBC walijelewesha kuanzishwa kwa shughuli hiyo muhimu ya kidemokrasia.

Iliarifiwa kwamba Kufikia saa kumi na mbili na takribani dakika ishirini hivi bado hakuna shughuli yoyote muhimu ilikuwa imeanza kufanyika katika kituo hicho licha ya wananchi kurauka mapema kabisa kujiandaa kupiga kura.

Waliingia kwa nguvu huku mageti yakiwa bado yamefungwa kwani hakuna aliyeruhusiwa kuingia.

Uwepo wa maafisa kwenye lango haukuwazuia kuingia kwa nguvu.

Wapiga kura wengi walikatishwa tamaa na ucheleweshaji na ukosefu wa mawasiliano kutoka kwa wafanyikazi wa IEBC.

Haya yanajiri huku tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ikitangaza Jumatatu jioni kuahirishwa kwa baadhi ya chaguzi za nyadhifa katika Kaunti ya Kakamega, Mombasa na sehemu fulani Pokot kwa kile kilichotajwa kuwa ni mkanganyiko wa karatasi za ugavana na ubunge.

Taarifa zaidi zinafuata….

 

Wapiga kura wengine walitishia kurudi nyumbani kabla ya kupiga kura zao.