Kazi ni mingi! Kanini Kega aonyesha akishona nguo baada ya kukubali kushindwa Kieni

Kanini alipakia picha inayoonyesha akishona fulana kutumia crotchet na uzi mweupe.

Muhtasari

•Licha ya masaibu yaliyokumba azma yake ya kuchaguliwa kwa muhula wa tatu Kanini alionekana mwenye furaha kubwa kwenye picha hiyo.

•Awali Jumatano Kanini alidokeza kuwa anatazamia kufungua ukurasa  mpya wa maisha yake baada ya kupoteza ubunge.

Image: FACEBOOK// KANINI KEGA

Mbunge wa Kieni anayeondoka Kanini Kega amewasisimua wanamitandao baada ya kupakia picha yake akishona nguo, masaa machache tu baada ya kukubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha mwaka huu.

Jumatano jioni, mkurugenzi huyo wa Kitaifa wa Uchaguzi wa  chama cha Jubilee alipakia picha inayoonyesha akishona fulana kutumia crotchet na uzi mweupe.

Licha ya masaibu yaliyokumba azma yake ya kuchaguliwa kwa muhula wa tatu Kanini alionekana mwenye furaha kubwa kwenye picha hiyo.

"Kazi ni mingi wadau!" Kanini aliandika chini ya picha hiyo aliyochapisha kwenye kurasa zake za mitandao kijamii.

Mbunge huyo anayeondoka alikuwa ameketi kwenye kiti huku akiwa amevalia mavazi ya kawaida.

Chapisho hilo lilijiri masaa machache baada yake kukubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha Jumanne.

Awali Jumatano Kanini alidokeza kuwa anatazamia kufungua ukurasa  mpya wa maisha yake baada ya kupoteza ubunge.

"Nafungua ukurasa mpya, wakati ukurasa mmoja ukifungwa mwingine unafunguliwa. Naelekea Bomas," Alisema kupitia Facebook.

Mwandani huyo wa rais Uhuru hata hivyo alibainisha kuwa bado yupo tayari kusukuma azma ya Raila kuwa rais.

Aidha aliwasuta wakazi wa eneo la Mt Kenya kwa kwenda kinyume na ombi la rais la kumuunga mkono Raila Odinga.

"Boss wangu na rafiki yangu. HE Uhuru Kenyatta Amri Jeshi, Ni suala la muda tu kwamba Mlima Kenya utagundua ulikuwa na maana kwao," Kanini alisema.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo kufuatia uungwaji mkono mdogo ambao  Raila amepata kutoka eneo hilo kulingana na matokeo yaliyotolewa tayari.

Hii ni licha ya hatua Rais Uhuru Kenyatta kuwataka kumuunga mkono Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais cha mwaka huu.

Uhuru amekuwa akiwahimiza wakazi wa eneo la Mlima Kenya kutomwangusha katika kuunga mkono kambi ya Azimio.