Kizaazaa Kilifi baada ya masanduku ya kura kuwasilishwa kama hayajafungwa

Sanduku la kura ya urais pekee ndilo lililokuwa limefungwa.

Muhtasari

•Masanduku matano ya kura yaliwasilishwa kama hayajafungwa katika kituo cha kuhesabia kura cha Kilifi Kaskazini.

• Suala hilo lilizua mvutano katika kituo cha kujumlisha kura na kusababisha wagombeaji wawili wa ugavana kukimbia katika kituo cha kujumlisha kura

Moja ya masanduku ya kura yaliyofika katika kituo cha kuhesabia kura cha Kilifi Kaskazini halijafungwa, Agosti 10, 2022.
Moja ya masanduku ya kura yaliyofika katika kituo cha kuhesabia kura cha Kilifi Kaskazini halijafungwa, Agosti 10, 2022.
Image: ELIAS YAA

Kizaazaa kikubwa kilizuka katika kituo cha kuhesabia kura cha Kilifi Kaskazini baada ya masanduku matano ya kura kuwasilishwa kama hayajafungwa.

Masanduku hayo kutoka kituo cha kupigia kura cha Bofa Primary yaliwasilishwa mwendo wa saa saba na dakika 40  usiku wa kuamkia Jumatano na Afisa Msimamizi.

Sanduku la kura ya urais pekee ndilo lililokuwa limefungwa.

Wananchi waliibua jambo wakati Afisa Msimamizi alipojaribu kufunga masanduku hayo katika kituo cha kuhesabia kura.

Ofisa huyo alisema alikosa kufunga masanduku hayo kwa sababu mvua ilikuwa ikinyesha na paa la darasa lililokuwa likitumika kama kituo cha kupigia kura lilikuwa likivuja.

“Sijavuruga matokeo, maajenti wote walisaini fomu zote na kushuhudia kila kitu,” alisema msimamizi huyo.

Sheria za uchaguzi zinawahitaji wasimamizi wa kura kufunga visanduku vyote vya kupigia kura kwa klipu zisizoweza kuharibiwa  baada ya upigaji kura, ambapo kukosa kufanya vile ni kosa la uchaguzi.

 Suala hilo lilizua mvutano katika kituo cha kujumlisha kura na kusababisha wagombeaji wawili wa ugavana kukimbia katika kituo cha kujumlisha kura. 

Mwaniaji wa ugavana wa ODM Gideon Mung'aro na mshindani wake wa cha Pamoja African Alliance Party George Kithi walisema hawatakubali matokeo hadi suala hilo lisuluhishwe. 

Afisa wa uchaguzi wa Kilifi kaskazini Khamis Tsumo aliwataka wagombea hao kumpa muda ili kupata ufafanuzi kutoka kwa afisa msimamizi. 

Wagombea hao pia walitaka kuhesabiwa upya ili kubaini ikiwa kura zililingana na matokeo ya Fomu 34A. 

 Hata hivyo, afisa msimamizi hakuweza kutoa fomu akidai alikuwa ameiweka kwenye sanduku la kura la urais lililofungwa. 

Msimamizi mwingine kutoka kituo cha kujumlishia shule ya msingi Korosho alileta sanduku moja la kura ambalo halijafungwa. 

Sanduku la kura la gavana lilikuwa na mihuri mitatu pekee huku mihuri mingine mitatu ikikosekana. 

Afisa msimamizi alieleza kwamba hakuwa amefunga sanduku hilo kwa sababu mihuri hiyo haikutosha.