Mmemwangusha rais Uhuru! Kanini Kega awaambia wakazi wa Mt Kenya baada ya kushindwa

Kega ni miongoni mwa wagombeaji ambao wamekubali kushindwa

Muhtasari

•Kanini Kega alisema wakati utafika ambapo eneo hilo litatambua umuhimu wa uungwaji mkono wa Uhuru.

•Kega ni miongoni mwa wagombeaji ambao wamekubali kushindwa hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa na IEBC.

Image: FACEBOOK// KANINI KEGA

Mbunge wa Kieni Kanini Kega amewasuta wakazi wa Mlima Kenya kwa kukosa kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.

Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook mnamo Jumatano, Kega alisema wakati utafika ambapo eneo hilo litatambua umuhimu wa uungwaji mkono wa Uhuru.

"Boss wangu na rafiki yangu. HE Uhuru Kenyatta Amri Jeshi, Ni suala la muda tu kwamba Mlima Kenya utagundua ulikuwa na maana kwao," Mbunge huyo wa mihula miwili alisema.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo kufuatia uungwaji mkono mdogo ambao mpeperushaji bendera wa Azimio Raila Odinga amepata kutoka eneo hilo kulingana na matokeo yaliyotolewa tayari.

Hii ni licha ya hatua Rais Uhuru Kenyatta kumuunga mkono Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais cha mwaka huu.

Uhuru amekuwa akiwahimiza wakazi wa eneo la Mlima Kenya kutomwangusha katika kuunga mkono kambi ya Azimio.

Kega, ambaye alikuwa anawania muhula wa tatu katika uchaguzi wa Agosti 9, ni miongoni mwa wagombeaji ambao wamekubali kushindwa hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

"Kufungua sura mpya, mlango mmoja ukifungwa mwingine unafunguliwa. Kuelekea Bomas," mbunge huyo alisema.

Kega alisema anatazamia kusonga mbele na kujaribu mambo mengine maishani.