Mtihani wa ikulu, nani mkombozi wa Kenya?

Kenya ina uwezo wa kujitegemea ikiwa ufisadi, ukabila na siasa chafu zitazimwa

Muhtasari

•Siasa  za Mwafrika mara nyingi zimehusishwa na kashfa, cheche na mgawanyiko katika misingi ya kikabila.

•Kinachowapa wakenya kiwewe ni kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwa ahadi za uongo. 

Image: THE STAR

Wananchi  wana haki kidemokrasia na kikatiba kuwateua viongozi  katika nyadhifa mbalimbali za uongozi.Ni fursa murwa waliokirimiwa kufanya mabadiliko kwa faida ya jamii zao.

Bara la Afrika kwa muda mrefu limetingwa na changamoto si haba licha ya hatua au mikakati kuwekwa ili kubadilisha hali mbaya.Utovu wa  tabia na  uongozi uliozorota umekuwa dondandugu tangu mkoloni kufunganya virago vyake.Kiongozi anayeshikilia uongozi ni zaidi ya hayawani.

Siasa  za mtu mweusi zimehusishwa na kashfa, cheche na mgawanyiko katika misingi ya kikabila.Vita baina ya jamii hasa husababishwa na tofauti za kisiasa na ugavi wa raslimali. Jamii zenye idadi kubwa ya wapiga kura  wakitaka kujinufaisha  pakubwa  huku wengine wakizama kwenye  lindi la akina pangu pakavu.

Taifa la Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo  kwa takaribani miongo sita bado saisa zao ni zile za ‘nitafanya hiki na kile’ almradi  mwanasiasa ashinde katika kinya’nga’nyiro.Vitu vya kimsingi bado ni shida kwa  wananchi kuvimudu. Ni dhahiri kwamba bado jamii halijaamua linahitaji nini na  kulifanyia kazi kwa madhumuni ya kutimiza ndoto zao.

Nchi ya Uswizi [ Sweden] ni kati ya  mataifa  ambazo raia wake hawakumbani na tatizo la uhaba wa maji, chakula, afya na lishe bora. Hii ni kwa sababu waliopewa uongozi walifahamu jukumu lao na daima hawakuchelea kutekeleza miradi endelevu. Hii ina maana hamna ufisadi katika  nchi hii na zile zingine zilizopiga hatua mbele kimaendeleo?

Tofauti na hulka za mwafrika, viongozi katika mataifa kama vile Sweden, Ujerumani, Amerika na zingine wamejizatiti zaidi kutumia asilimia kubwa  ya hela zilizotengewa afisi zao katilka kutekeleza maendeleo.

Kulingana na Joseph Nyasani na Michael Todaro ambao ni wataalam wa maswala ya jamii na maendeleo,wawili hawa wanakubaliana katika tafiti zao kwamba mwafrika hutumia karibu kila kitu kuhudumia tumbo na familia zao pasi kujali raia wanaotegemea hudumu za serikali

Serikali  ya Jubilee inayoondoka mamlakani baada ya  kura za uchaguzi, ilijishughulisha pakubwa katika kuboresha  miundomsingi kama vile barabara, daraja, miradi ya maji miongon i mwa  zingine.Hii huchangia katika maendeleo ya jamii katika kila sekta.

Lakini Profesa Nyasani, katika  tafiti zake  katika mbinu za kustawisha Kenya, anasema kujenga barabara na  miundomsingi zingine si tosha wakati wakazi wanalala njaa. Anaelezea kuwa  uzalishaji wa chakula na wananchi kuwa na uhuru kubadilisha hali na maisha yao ndo inayowapa furaha.

Katika  kampeni  za wagombea kiti cha urais kutoka muugano wa  Azimio la umoja one- Kenya[Raila Odinga], Kenya Kwanza[William Ruto], chama cha Agano[ David Mwaure], na Roots Party[Prof Wajackoyah], vyote  vilishamiri ahadi za kuboresha uchumi na kutengeneza nafasi zaidi za ajira kwa vijana.

Kinachowapa wakenya kiwewe ni kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwa ahadi za uongo. Kwa mfano zaidi ya asilimia 35 ya wanafunzi kutoka vyuo vya kiufundi na vikuu hawakuripoti shuleni kwa sababu za ukosefu wa karo na pesa kumudu mhitaji mengine.

Takwimu zaonyesha kwamba   zaidi ya asilimia 23.7 hawana uwezo wa kukidhi mahitaji yao. Ukosefu wa lishe na afya bora ikichangia katika idadi ya ugonjwa wa utapiamlo na vifo.Hawa watu takribani million ishirini wanahitaji  kukomolewa toka kwenye jinamizi linalowasibu haraka iwezekanavyo.

Kuna haja ya taifa hili kujifunza kutoka kwa mataifa kama vile Uchina yaliyopiga hatua mbele kimaendeleo. Uchina  imeweza kuwakomboa  watu kuzidi milioni 800 kutoka kwenye umasikini. Sera  na utekelezwaji wa miradi ulishabikiwa na raia wengi ambao hali yao ilikuwa heri ya jana. Leo hii taifa la China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uzalishaji na teknologia.

Kenya ina uwezo wa kujitegemea ikiwa ufisadi, ukabila na siasa chafu zitazimwa ili kila mtu ajitose katika kazi na kuzidisha ari ya kuboresha uchumi. Hii si jukumu la serikali pekee, linahitaji uwajibikaji kutoka mashrika za kibinafsi na raia kwa ujumla.

Na ndiposa safu hiii  inapiga darubini kuhusu kibarua cha atakayemrithi  rais Uhuru Kenyatta  baada ya uchaguzi . Taifa hili haliitaji wenye porojo  ambao kamwe hamna matendo. Kenya  inahitaji Thomas Sankara, Sere Sekama na Hayati rais wa Tanzania, Pombe Magufuli ili kunyorosha na kurudisha nidhamu serikalini.

Sera zao ziwe za kuleta mtazamo mpya katika jamii ya mkenya  na inayolenga kuweka taifa hili miongoni mwa mataifa yenye ruwaza ya Afrika 2063. Tusiruhusu siasa na mikwaruzano kusambaratisha  jamii yetu kama  vile nchi za Nigeria, Rwanda, na Congo  ambazo  zingine hadi wa leo zinashuhudia  michafuko