Didmus atangazwa mshindi Kimilili licha ya kutojulikana aliko baada ya kudaiwa kuua

Hakuna mgombea yeyote ambaye alifika katika kituo cha kujumuisha kura kushuhudia matangazo ya matokeo.

Muhtasari

•Barasa alitangazwa mshindi wa kinyang'anyiro cha Kimilili Jumatano usiku baada ya kujizolea kura 26, 861 na kuwabwaga chini washindani wake watatu.

•Polisi wanaamini kuwa Barasa alitorokea Uganda baada ya madai ya kumuua msaidizi wa mmoja wa mpinzani wake

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Image: MAKTABA

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amefanikiwa kuhifadhi kiti chake baada ya kunyakua ushindi katika kinyang'anyiro cha Jumanne.

Barasa ambaye kwa sasa hajulikani aliko kufuatia madai ya mauaji alitangazwa mshindi wa kinyang'anyiro cha Kimilili Jumatano usiku baada ya kujizolea kura 26, 861 na kuwabwaga chini washindani wake watatu.

Alikuwa akimenyana na Peter Makokha wa ODM, Erastus Muchimudi wa Jubilee na Brian Khaemba wa DAP-K.

Hakuna yeyote kati ya wagombea wanne hao ambaye alifika katika kituo cha kujumuisha kura kushuhudia matangazo ya matokeo.

Polisi wanaamini kuwa Barasa alitorokea Uganda baada ya madai ya kumuua msaidizi wa mmoja wa mpinzani wake, Brian Khaemba mnamo siku ya uchaguzi.

Maafisa wanaoshughulikia kesi hiyo walisema mbunge huyo kufikia Jumatano alikuwa hajasalimisha kama alivyoagizwa.

Barasa, ambaye kufuatia ushindi huo atahudumu kwa muhula wa pili  ni mmiliki wa bunduki aliyeidhinishwa.

Mbunge huyo anadaiwa kumpiga risasi Bw Brian Olunga kufuatia ugomvi ulitokea katika kituo cha kupigia kura cha Chebukwabi Jumanne jioni. Olunga alifariki katika hospitali ya Kimilili Subcounty alipokuwa akipokea matibabu ya dharura.

Jumanne, mkuu wa DCI wa Bungoma Joseph Ondoro alisema Barasa alizozana na Khaemba, hatua ambayo ilimfanya  mpinzani huyo wake kuondoka na kuelekea kwenye gari lake.

"Barasa alimfuata akiwa na wanaume wanne na kuwaamuru wasimruhusu (Khaemba) kuondoka mahali hapo lakini dereva wa Khaemba Joshua Nasokho alikaidi amri hiyo na kuwasha gari," alisema Ondoro.

Hapo ndipo Barasa alipochomoa bastola na kumlenga msaidizi wa Khaemba Brian Olunga na kumpiga risasi ya paji la uso.Olunga alifariki katika hospitali ya Kimilili Subcounty alipokuwa anapokea matibabu ya dharura.

Ondoro alisema wanamtafuta Barasa kwa ajili ya kuhoji kuhusu tukio hilo.

“Amekimbia lakini tunamtafuta. Ajisalimishe,” alisema.