ODM yanyakua viti vinne vya ubunge huko Homa Bay

Caroli Omondi, Martin Owino, Ongondo Were na Millie Odhiambo walitangazwa wabunge wateule baada ya kuwabwa washindani wao.

Muhtasari

•Chama cha ODM kinaelekea kupata ushindi mkubwa katika viti vyote vinane vya ubunge katika kaunti ya Homa Bay.

•Millie Odhiambo alishinda kwa kumbwaga chini mpinzani wake mkuu James Akali baada ya kupata kura 27,130.

Mbunge wa Ndhiwa Martin Owino akionyesha cheti chake cha muda baada ya kunyakua kiti hicho mnamo Agosti 10,2022
Mbunge wa Ndhiwa Martin Owino akionyesha cheti chake cha muda baada ya kunyakua kiti hicho mnamo Agosti 10,2022
Image: ROBERT OMOLLO

ODM inaelekea kupata ushindi mkubwa katika viti vyote vinane vya ubunge huko Homa Bay baada ya wagombea wanne wa chama hicho kutangazwa washindi.

Wagombea hao ambao ni pamoja na Caroli Omondi (Suba Kusini), Martin Owino (Ndhiwa), Ongondo Were (Kasupil) na Millie Odhiambo (Suba Kaskazini) walitangazwa kuwa wabunge wateule baada ya kuzoa kura nyingi kuliko washindani wao.

Caroli aliibuka mshindi baada ya kupata kura 25,805. Stephen Sangira ambaye aligombea kama mgombea binafsi alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura 14,396.

Wagombea wengine Julius Opala na Omedo Misama walipata kura 187 na 161 mtawalia.

Caroli aliwapongeza wakazi kwa kumpigia kura kumrithi mwenyekiti wa kitaifa wa ODM John Mbadi.

Caroli ataingia kwa mara ya kwanza katika Bunge la Kitaifa baada ya kujaribu mara tatu lakini akashindwa na Mbadi.

"Ninawashukuru watu wa Suba Kusini kwa heshima waliyonitendea. Nitawafanyia kazi kwa bidii ili kuhakikisha tunalipeleka eneo hili katika kilele cha maendeleo," Caroli alisema.

Suba Kusini ina wapiga kura 54,839 waliojiandikisha. Furaha kama hiyo hiyo iligubika uso wa Millie Odhiambo ambaye alichaguliwa mara ya tatu kurejea bungeni.

Millie alishinda kwa kumbwaga chini mpinzani wake mkuu James Akali baada ya kupata kura 27,130.

Akali ambaye alitafuta kiti hicho kwa tiketi ya Federal Party of Kenya alipata kura 18,151.

Matokeo ya Suba Kaskazini yalitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa IEBC Peter Onyango.

Onyango aliwashukuru wanasiasa kwa kudumisha amani wakati wa kampeni.

Katika eneo bunge la Ndhiwa, mbunge wa sasa Owino alinyakua kiti hicho baada ya kumshinda aliyekuwa mbunge Agostino Neto.

Owino alipata kura 31,834 huku Neto wa chama cha United Green Movement (UGM) akipata kura 20,835. Mgombea huru Michael Agwanda alipata kura 17,765 na kuibuka nambari tatu.

"Wananchi wa Ndhiwa wamethibitisha mshikamano wao na chama cha ODM. Tutaanza ajenda yetu ya maendeleo," Owino alisema.

Ndhiwa ina wapiga kura 96,734 waliojiandikisha. Mbunge wa Kasipul Were aliahidi kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika eneo bunge hilo baada ya kupata kura 40,210 na kuwashinda wagombeaji wengine 11 ambao ni pamoja na Grace Okinda na George Otieno.

Okinda alipata 3,100 huku Otieno akipata kura 2100.

Wagombea wengine wa ubunge wa ODM Peter Kaluma wa eneo bunge la Homa Bay Town, Adipo Okuome ((Karachuonyo), Lilian Gogo (Rangwe) na Eve Obara (Kabondo Kasupil) pia walikuwa wamejitokeza kuhifadhi viti vyao.

Walikuwa wakiongoza katika matokeo ya muda katika maeneobunge yao.

Ushindi wao unaonyesha kuwa ODM bado ni chama chenye nguvu huko Homa Bay.