Wabunge Kj, Aladwa na Kajwang wachaguliwa tena Nairobi

Kufuatia ushindi wa KJ, naibu rais William Ruto amenyakua kiti chake cha pili Nairobi.

Muhtasari

•Kj wa United Democratic Alliance(UDA) alipata kura 26,304 dhidi ya Waweru wa Jubilee kura 22,773.

•George Aladwa amechaguliwa tena baada ya kupata 32,332 akimshinda mpinzani wake wa UDA Antony Waithaka aliyepata kura 28,545.

Mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie
Image: FACEBOOK// JOHN KIARIE

Mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie amechaguliwa tena huku akimshinda aliyekuwa mbunge Dennis Waweru.

Kj ambaye alikuwa akitetea kiti chake kwa tiketi ya United Democratic Alliance(UDA) alipata kura 26,304 dhidi ya Waweru wa Jubilee kura 22,773.

Wakati huo huo, mbunge wa Ruaraka wa awamu ya pili Tom Kajwang pia amechaguliwa tena kwa muhula wake wa tatu.

Alimshinda mpinzani wake mkuu, Boaz Chelugut wa UDA.

Kufuatia ushindi wa KJ, Naibu Rais William Ruto amenyakua kiti chake cha pili Nairobi baada ya Benjamin Mwangi (Embakasi Central) kushinda.

Pia, Mbunge wa Makadara George Aladwa amechaguliwa tena baada ya kupata 32,332 akimshinda mpinzani wake kutoka UDA, Antony Waithaka aliyepata kura 28,545.

Pia Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino amechaguliwa tena, Felix Odwuor almaarufu Jalango (Langata) na Peter Ochieng wa Kibera walitangazwa washindi.

Wenzake George Theuri (Embakasi Magharibi) na Nixon Korir (Lang'ata) walikubali Jumatano asubuhi.

Mark Mwenje wa Jubilee ndiye mbunge anayekuja wa Embakasi Magharibi.