•Bahati aliibuka wa tatu kwa kura 8,166, nyuma ya mbunge wa sasa Antony Oluoch na Billian Ojiwa.
•Mwanamuziki huyo alifichua kwamba alikuwa ametumia takriban shilingi milioni 33 katika kampeni zake.
Mwimbaji maarufu Kelvin Kioko almaarufu Bahati amefeli katika jaribio lake la kuwa mbunge afuataye wa Mathare.
Bahati aliibuka wa tatu kwa kura 8,166, nyuma ya mbunge wa sasa Antony Oluoch na Billian Ojiwa.
Oluoch ambaye aliwania kwa tiketi ya ODM aliifadhi kiti chake baada ya kuzoa kura 28,098 katika kinyang’anyiro hicho kilichokuwa na mvutano mkali ulioshuhudia mpinzani wake wa karibu Billian Ojiwa akipinga zoezi la kuhesabu kura.
Ojiwa ambaye aligombea kwa tikiti ya UDA alipata kura 16,912. Ameapa kupinga zoezi hilo mahakamani.
Oluoch ambaye atahudumu eneo bunge hilo kwa muhula wa pili ameahidi kushirikiana na washindani wake kupambana na umaskini eneo hilo.
"Ninawaalika washindani wangu wote wenye uwezo ili tufanye kazi kwa ajili ya watu wetu," Oluoch alisema.
Siku chache kabla ya uchaguzi kufanyika, mwanamuziki huyo alifichua kwamba alikuwa ametumia takriban shilingi milioni 33 katika kampeni zake.
“Nimetumia takriban milioni 33 kwenye kampeni za uchaguzi, napata kuungwa mkono na watu wema, bajeti yangu siku ya uchaguzi ni milioni 10. Kampeni za kuwania nafasi ya Ubunge zinagharimu zaidi ya Milioni 50," Alisema.