Kawira Mwangaza awabwaga chini Kiraitu, Linturi na kunyakua ugavana wa Meru

Mwangaza alipata kura 209,148 huku Linturi akiibuka wa pili kwa kura 183,859.

Muhtasari

•Mwangaza ambaye aliwania kama mgombea huru aliwabwaga chini Kiraitu Murungi na Seneta Mithika Linturi kunyakua kiti hicho.

•Kawira alimshukuru Mungu, mumewe Murega Baichu, naibu wake Isaac Mutuma na jamii ya Wameru kwa kuamini uongozi wake wa LL.

Gavana mteule wa Meru Kawira Mwangaza
Gavana mteule wa Meru Kawira Mwangaza
Image: HISANI

Mwakilishi wa wanawake wa Meru anayeondoka Kawira Mwangaza ameshinda kiti cha ugavana wa kaunti hiyo.

Mwangaza ambaye aliwania kama mgombea huru aliwabwaga chini Kiraitu Murungi na Seneta Mithika Linturi kunyakua kiti hicho.

Alipata kura 209,148 huku Linturi akiibuka wa pili kwa kura 183,859.

Kiraitu ambaye ndiye gavana anayeondoka alikuwa wa tatu kwa kura 110,814.

Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho, Kawira alimshukuru Mungu, mumewe Murega Baichu, naibu wake Isaac Mutuma na jamii ya Wameru kwa kuamini uongozi wake wa LL.

"Ninawaahidi, Meru itakuwa kaunti bora zaidi. Kutakuwa na miradi ya maendeleo endelevu. Tunaanza kufanya kazi sasa hivi na ninaamini Meru itakuwa bora zaidi nchini Kenya. Nitawaunganisha Wameru wote licha ya makabila yao madogo," Kawira alisema Ijumaa jioni.

Kawira ambaye aliandamana na mbunge mteule wa Tigania Mashariki Mpuru Aburi aliwataka wabunge wa Meru kufanya kazi pamoja kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa Kaunti hiyo.

"Nawakaribisha wabunge wote kuungana nami kwa umoja, hii pia itaboresha maendeleo. Nitakuwa mtumishi mwaminifu kuitetea Meru na wananchi wake," Kawira alisema.