Majaribio 200 ya kudukua server zetu yalifanywa usiku- IEBC

Majaribio hayo yalifanywa kati ya saa nne usiku wa Alhamisi na saa mbili asubuhi ya Ijumaa.

Muhtasari

•Wakati mmoja wakala wa moja ya vyama kuu alijaribu kudukua mfumo wa IEBC kutoka ndani ya Bomas.

•Mkurugenzi Mtendaji Hussein Marjan alisema iebc ina ulinzi tosha kuhakikisha usalama wa fomu za matokeo na data zinazozalishwa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein, Kamishna Francis Wanderi, Mwenyekiti Wafula Chebukati na Makamu Mwenyekiti wa tume Juliana Cherera wakati wa kutolewa kwa matokeo ya Urais katika ngazi ya eneo bunge la Bomas of Kenya mnamo Agosti.
Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein, Kamishna Francis Wanderi, Mwenyekiti Wafula Chebukati na Makamu Mwenyekiti wa tume Juliana Cherera wakati wa kutolewa kwa matokeo ya Urais katika ngazi ya eneo bunge la Bomas of Kenya mnamo Agosti.
Image: ENOS TECHE

Majaribio 200 ya udukuzi yalikuwa yamefanywa kwenye server za IEBC kati ya saa nne usiku wa Alhamisi na saa mbili asubuhi ya Ijumaa..

Radio Jambo iligundua kuwa wakati mmoja, wakala wa moja ya vyama kuu alijaribu kudukua mfumo wa IEBC kutoka ndani ya Bomas.

Jaribio hilo hata hivyo liligunduliwa na kompyuta yake ndogo ikachukuliwa.

Akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Bomas siku ya Ijumaa, Mkurugenzi Mtendaji wa tume ya uchaguzi Hussein Marjan alisema wana ulinzi tosha kuhakikisha usalama wa fomu za matokeo na data zinazozalishwa.

Marjan alikuwa akijibu madai kwamba baadhi ya watu walijaribu kudukua mfumo ili kuweka hesabu na kuathiri matokeo.

"Hakuna kitu kama hicho kimetokea. Tulitarajia watu wangejaribu kupenya kwenye mfumo na tukaweka ulinzi. Tunajua watu hawalali, wanataka kuhakikisha mifumo yetu iko chini," alisema.

"Tunaihakikishia nchi nzima kuwa mifumo yetu iko salama. Ikiwa una shaka, zungumza nasi ili kuongeza mfumo wa usalama."