Msimamizi wa uchaguzi wa Embakasi East hajulikani aliko- Chebukati

Afisa Daniel Musyoka alitoweka siku ya Alhamisi mwendo wa saa nne kasorobo asubuhi.

Muhtasari

•Musyoka alikuwa katika kituo cha kujumlisha kura cha East African School of Aviation alipotoweka mwendo wa saa nne kasorobo asubuhi.

•Naibu wa msimamizi huyo sasa amechukua majukumu yake.

Image: ANDREW KASUKU

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebuakti ametangaza kuwa msimamizi wa uchaguzi wa eneo la Embakasi Mashariki hajulikani aliko.

Musyoka ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha East African School of Aviation hakuwepo kwa ajili ya kukabidhi cheti kwa washindi siku ya Alhamisi.

MCAs waliochaguliwa na mbunge mteule Babu Owino walikabidhiwa vyeti vyao na afisa mwingine wa IEBC aliyesimama kwa niaba ya Musyoka.

Chebukati alipokuwa akihutubia wanahabari alisema Musyoka alitoka nje kupiga simu mnamo Alhamisi, Agosti 11 mwendo wa saa nne kasorobo asubuhi.

"Familia ya Musyokas na Tume wamekuwa wakijaribu kumfikia bila mafanikio. Ripoti ya mtu aliyepotea imetolewa katika kituo cha polisi cha Embakasi," Chebukati alisema.

Naibu wa msimamizi huyo sasa amechukua majukumu yake.

Siku ya Jumanne, wanahabari waliojaribu kumfikia Musyoka mchana waliambiwa kwamba alikuwa ametoka kuchukua 'mapumziko.'

Kutokuwepo kwake kulizua tafrani ukumbini baada ya umati kuanza kutaka arejeshwe ili kutangaza matokeo.