UDA yanyakua viti vyote vinne vya ubunge Kirinyaga

Chama hicho pia kilinyakua viti 17 kati ya 20 vya MCA kote kaunti hiyo.

Muhtasari

•George Kariuki wa Ndia, Gichimu Githinji wa Gichugu, Gachoki Gitari (Kirinyaga ya kati) na mbunge mteule wa Mwea kwa awamu ya kwanza Mary Maingi walipata ushindi mkubwa.

•Mwakilishi wa wanawake, gavana na seneta bado hawajatangazwa na lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba UDA imenyakua nyadhifa hizo kwa ushindi mnono.

Mbunge mteule wa Kirinyaga Gachoki akipokea cheti chake cha IEBC kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi eneo bunge James Maingi
Mbunge mteule wa Kirinyaga Gachoki akipokea cheti chake cha IEBC kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi eneo bunge James Maingi
Image: WANGECHI WANG'ONDU

Chama cha naibu rais William Ruto cha UDA kinaelekea kupata ushindi mkubwa katika kaunti ya Kirinyaga baada ya kusajili matokeo bora katika nyadhifa zote nne za uwakilishi wa bunge.

Katika matokeo ambayo yalitangazwa Jumatano na Alhamisi, katika vituo mbalimbali vya kujumlisha kura katika maeneobunge manne, George Kariuki wa Ndia, Gichimu Githinji wa Gichugu, Gachoki Gitari (Kirinyaga ya kati) na mbunge mteule wa Mwea kwa awamu ya kwanza Mary Maingi walipata ushindi mkubwa, thibitisho kuwa chama hicho ndicho maarufu zaidi na chenye misingi mikuu huko Kirinyaga.

Katika eneobunge la Gichugu, mbunge wa sasa Gichimu Githinji alitangazwa mshindi Alhamisi baada ya kuwashinda wapinzani wake wengine 9 kwa jumla ya kura 33,889. Mpinzani wake wa karibu Peterson Njomo Muchira aliibuka wa pili kwa jumla ya kura 15,069.

Eneo bunge hilo lina jumla ya wapiga kura 65,736 waliojiandikisha.

Akizungumza baada ya kutunukiwa cheti cha ushindi, Gichimu aliwashukuru wakazi wa eneobunge hilo kwa kumpa nafasi ya pili.

Aliahidi kutumia nafasi yake kuwafanyia kazi wakazi wote wa Gichugu bila kujali ni nani anayemuunga mkono au la.Katika eneo la Kirinyaga ya kati, Gachoki Gitari alinyakua kiti hicho baada ya kuwa kwenye baridi ya kisiasa kwa miaka mitano iliyopita.

Gitari, alinyakua kiti hicho kwa jumla ya kura 34,074 dhidi ya mpinzani wake wa karibu na mbunge wa sasa Munene Wambugu ambaye alipata kura 22,591 baada ya kuwania kwa tikiti ya chama cha Jubilee.

Gitari katika hotuba yake ya kukubalika aliwashukuru maafisa wa tume la uchaguzi kwa kudumisha weledi katika kazi zao.

Vile vile aliwashukuru wafuasi wake kwa kujitokeza kwa wingi kumpigia kura.Aliahidi kutovunja imani waliyoweka kwake badala yake akaahidi kuwatumikia kwa uwajibikaji kadri ya uwezo wake.

Katika eneo la Mwea lenye watu wengi, Mary Maingi alitangazwa kuwa mbunge mteule baada ya kupata kura 50,667 dhidi ya Kabinga Wachira wa Jubilee aliyepata kura 31,735.

Mnamo Jumatano, George Kariuki wa UDA alitangazwa kuwa mbunge mteule wa Ndia baada ya kupata kura 25,031.

Kando na hayo, chama hicho pia kilichukua viti 17 kati ya 20 vya MCA kote kaunti hiyo. Nyingine tatu zilishinda na The service party (TSP) na Jubilee party.

Washindi wa nyadhifa za mwakilishi wa wanawake, ugavana na useneta bado hawajatangazwa na IEBC lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba UDA imenyakua nyadhifa hizo kwa ushindi mnono.